Tuesday, 30 April 2013

WANAUME MBEYA WAJITOKEZA KWA WINGI KUPIMA KISUKARI NA SHINIKIZO LA DAMU KUFUATIA BIMA YA AFYA KUPIMA BURE UWANJA WA SOKOINE IKIWA NI MAADHIMISHO YA MEI MOSI INAYOFANYIKA KITAIFA MKOANI MBEYA HUKU WANAWAKE WAKITAKA KUPIMA UKIMWI


BAADHI YA MAAFISA WA MFUKO WA BIMA YA AFYA MKOANI MBEYA WAKIWA KWENYE BANDA LA UPIMAJI WA AFYA BURE, HUDUMA INAYOTOLEWA NA MFUKO HUO AMBAPO BAADA YA KUPIMWA WANANCHI HUPEWA USHAURI.

Na Mgalula Joseph, Mbeya
WANAUME mkoani Mbeya wengi wamejitokeza kupima magonjwa ya Kisukari na shinikizo la damu huku wanawake wakijitokeza kwa wingi kupima VVU.
Hali hiyo imebainika katika banda la mfuko wa taifa wa bima ya afya(NHIF)lililopo katika uwanja wa Sokoine ambako mfuko huo unatoa huduma ya upimaji bure ikiwa ni kuazimisha siku kuu ya wafanya kazi (Mei mosi) inayofanyika kitaifa mkoani hapa na mgeni rasmi ni Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza na Mtandao wa www.kalulunga.blogspot.com afisa uhakiki na ubora wa mfuko huo, Dr. Lucas Gama, alisema kuwa wananchi wengi wameendelea kujitokeza kupima afya zao tangu jana wakiwemo wanawake na wanaume hasa vijana.
‘’Wanajitokeza kwa wingi, lakini wanawake wengi wanaokuja wanasema wanataka kupima Ukimwi wakati wanaume wanaokuja wanauliza tunapima nini na tukiwaambia tunapima Kisukari na shinikizo la damu wanaongezeka kuja kupima’’ anasema Dr. Gama.
Alisema kuwa imejengeka tabia kwa baadhi ya wananchi kuona kuwa Ukimwi ni ugonjwa hatara wakati ugonjwa huo hauuwi haraka tofauti na magonjwa kama kisukari na shinikizo la damu(BP).
‘’Magonjwa haya ni magonjwa hatari na yanaua haraka kuliko Ukimwi, jana tumewapata wagonjwa watatu ambao wana sukari 200 jambo ambalo ni hatari sana na tumewapa ushauri na hapo utagundua kuwa watu wanatembea na majeneza’’ alisema Dr. Gama.
Alifafanua kuhusu magonjwa hayo kuwa shirika la afya duniani(WHO), linasema kuwa Sukari na shinikizo la damu ni viashiria vya afya ya mtu, ambapo sukari ikiwa 7 kwenda chini ni sukari ya kawaida ila kwenda juu mtu akiwa hajala ni hatari.
Kwa upande wake afisa wa NHIF mkoa wa Mbeya Reginald Kileo, alisema kuwa mfuko huo umeona umuhimu wa kutoa huduma hiyo bure ili  wananchi waweze kuwa na mazoea ya kupima afya zao.
‘’Watu wanatembea na makaburi lakini hawajui, hivyo ni muhimu serikali ikaendelea kutoa elimu kwa wananchi kujitokeza kupima afya zao na iwe bure’’ alisema Kileo.
Mwananchi Agness Mojo mkazi wa Soweto na Jackson Matengula mkazi wa Uyole ambao ni baadhi ya waliojitokeza kupima afya zao walisema kuwa wanashindwa kupima afya zao hospitali kutokana na kutozwa fedha huku mapokezi yakiwa hayaridhishi.
Upimaji huo wa afya bure, unaishia kesho siku ya Mei mosi katika viwanja vya Sokoine kupitia mfuko huo wa taifa wa bima ya afya.

TANGAZO PROGRAMU MAALUMU YA KUWAANDAA WATAHINIWA KUFANYA/KURUDIA MTIHANI WA TAIFA KIDATO CHA NNE-2013/2014



CHUO KIKUU TEOFILO KISANJI
  
KURUGENZI YA ELIMU ANUAI

PROGRAMU MAALUMU YA KUWAANDAA WATAHINIWA  KUFANYA/KURUDIA MTIHANI WA TAIFA KIDATO CHA  NNE-2013/2014

Chuo Kikuu Teofilo Kisanji (TEKU) kinakaribisha  maombi kutoka
Kwa watahiniwa wote waliomaliza Kidato cha Nne kujiunga na
program maalumu.
Lengo la programu hii maalumu ni kuwawezesha watahiniwa
wanaopenda kujiunga na kidato cha Tano pamoja na kozi
mbalimbali za cheti na stashahada kupata sifa itakazowawezesha
kuendelea na masomo kwangazi husika.
Masomo yataanza tarehe 30/4/2013 na yataendeshwa kwa muda
wa miaka miwili tu.  Mwisho wa kupokea maombi ni tarehe 28 /4/
2013 na usajili utafanyika tarehe 28/4/203. 
  
Masomo yatakayofundishwa ni kama ifuatavyo:

· Uraia (Civics)
· Historia (History)
· Jiografia (Geography)
· Kiswahili
· Kiingereza (English)
· Fizikia (Physics)
· Kemia (Chemistry)
· Biolojia (Biology)
· Hisabati (Basic Mathematics)
· Fasihi ya Kiingereza (Literature in English)
Sifa za Mwombaji:
Muombaji awe na namba ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne
Ada kwa mwaka ni Tsh. 430,000/=
Malipo haya yanalipwa moja kwa moja  kwenye akaunti za Chuo
Kikuu Teofilo Kisanji hayajumuishi gharama za
malazi, chakula na usafiri.
 Akaunti za Chuo ni kama ifuatavyo:

Teofilo Kisanji University
NBC   Account no. 016103001650
STANBIC Account no. 0140015028101
CBA Account no. 0300786000
CRDB account no. 01J1065895000
Fomu zinapatikana chuoni, eneo la Kitalu  T,  Mbeya mjini na vilevile mwombaji anaweza kuzipata kutoka katika Tovuti ya chuo: www.teku.ac.tz
Maombi yatumwe kwa:
Mkurugenzi,
Kurugenzi ya Elimu Anuai
Chuo Kikuu Teofilo Kisanji
Kampasi ya Zamani, Kitalu. T
S.L.P. 1104
Mbeya
TANZANIA
Simu:  +2550252502682 
Faksi: 2550252503721
Baruapepe: info@teku.ac.tz
Tovuti:   www.teku.ac.tz

Mbunge Mlokole Ataka Jumapili Isitumike Kupiga Kura

 

Mhe. Asumpta akiwa na Mhe. "Sugu" Wakibadilishana Mawazo.
Mama Mzazi wa Kundi Maarufu Katika Anga la Muziki wa Injili alimaarufu kama Jsiters.Mbunge wa Nkenge, Asumpter Mshama (CCM) ameitaka Serikali kutoa tamko la lini itaacha utaratibu wa kutumia siku ya Jumapili kwa ajili ya kupiga kura.
Mbunge huyo alihoji iwapo Serikali haioni tatizo kuwadhulumu baadhi ya waumini muda wao na kwamba jambo hilo limekuwa likisababisha baadhi ya watu kukimbilia kufanya ibada na huku wakishindwa kupiga kura.
“Kitendo cha kufanya uchaguzi wa kitaifa siku za Jumapili kinasababisha baadhi ya watu kushindwa kupiga kura jambo linalowanyima haki yao ya kikatiba,” alisisitiza Mshama.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge William Lukuvi, alikiri kuwa sheria za uchaguzi pamoja na kanuni zake, haziainishi siku maalumu ya iliyoteuliwa kwa ajili ya kupiga kura.
Lukuvi alisema kuwa uamuzi wa Serikali kuteua siku ya Jumapili kwa ajili ya kupiga kura ulitokana na sababu kuwa ni siku ambayo Watanzania wengi hawaendi kufanya kazi hivyo kuwa na fursa katika zoezi la kupiga kura.
Hata hivyo alikiri kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa watu wengi kuhusu siku ya Jumapili wakitaka ibadilishwe ili isitumike kwa ajili ya kupiga kura lakini pia Serikali inatambua kwa dhati kuwa ni siku maalumu kwa ajili ya waumini wa dini ya Kikristo.
Alisema suala hilo litafanyiwa kazi katika marekebisho ya Katiba Mpya ambayo Tanzania inatarajia kuipataKatiba Mpya kuanzia Aprili mwakani wakati uchaguzi mkuu utafanyika Oktoba 2015 .

Source: Mwananchi.


SABABU 5 KWANINI UPENDO HAUTOSHI KUJENGA MAHUSIANO BORA

 

Ukisoma kwa kutafakari makala hii utagundua kuwa kuweza kujifahamu sisi wenyewe vema, kuweza kujitawala sisi wenyewe, na pia kuweza ‘kuwasoma’ vema wenzi wetu , ni mambo ya msingi sana ili upendo tulionao uweze kudumisha mahusiano.  Msisitizo ni kwamba, pamoja na ukweli kuwa upendo ni kitu cha muhimu katika mahusiano, makala hii inaeleza kuwa kutegemea upendo pekee kama nguzo kuu ya mahusiano bora kunaweza kuwa jambo la hatari kwa mahusiano, kwa sababu zifuatazo:-

1. Binadamu ni kiumbe huru: Ni muhimu kukumbuka hili hasa kama unadhani kwakuwa unampenda fulani na umemuonyesha mapenzi yako yote basi hicho ni kama kifungo kwake kuwa hatoweza kutoka katika penzi lenu. Kwa asili binadamu ni huru, na anaweza kuamua kuutumia uhuru wake kufanya maamuzi mengine yoyote tofauti na unavyofikiri ni lazima afanye.  Kwa kuwa pia ni mbinafsi, basi kama upendo wako wote kwake hauendani na yale anayotazamia , unaweza kukuta ameshindwa kukaa katika penzi , ambalo kwa watu wengi wanaona kuwa ni penzi zito.

2. Binadamu ni mbinafsi kwa asili: Binadamu kwa asili huangalia maslahi yake kwanza kabla ya kuangalia ya mwingine. Mfano dhahiri wa ubinafsi huu ni pale inapotokea ajali , mara nyingi mtu huwaza kujiokoa mwenyewe kwanza kabla ya kufikiria wa karibu yake. Tumesikia habari za mama mzazi kuacha kitoto kichanga ndani wakati moto ukiendelea na yeye kutoka nje. Kuna habari pia za mama kumtumia mtoto wake kama ‘kifaa’ cha kuvunjia kioo cha gari , ili aweze kujiokoa, pale ambapo ajali ilitokea. Hivyo upendo tuu pekee hautoshi kumfanya mtu aendelee kukaa katika ndoa au mahusiano kabla ya ndoa (uchumba), ni muhimu yawepo mambo mengine yenye manufaa kwa mtu husika.

3. Binadamu ana mahitaji mengi  na yasiyo na kikomo:  Mwenza wako ana mahitaji mengi na yanaongezeka na kubadilika siku hadi siku kutegemeana na mabadiliko mbalimbali kama vile hali ya hewa, aina ya kazi, watu anaokutana nao, mabadiliko ya teknolojia, mabadiliko ya kiuchumi n.k. Upendo wenu, hausimamishi mahitaji haya yasitokee, na kwamba upendo pekee hauwezi kuwa jibu la kutimiza mahitaji hayo. Inahitajika bidii katika kujituma kujiletea kipato, kuwa na mawasiliano bora kati yenu, kutambua mabadiliko na kuchukua hatua kabla mabadiliko hayajawabidilisha, na zaidi sana muweze kuwa na utamaduni wa kupanga mambo pamoja na kuwa waaminifu katika kutimiza yale mnayopanga. 
Chukulia mfano, wa wanandoa walioishi vema kwa miaka 5 ya ndoa, halafu ndoa ikaanza kulemaa kwa kuwa mmoja wao anaona hakuna uwajibikaji katika kumsaidia mwengine kujiendeleza kielimu, kibiashara, au kutimiza ndoto nyingine ambayo mwanandoa amekuwa nayo.

4. Binadamu wengi wanashindwa kujitawala:  Uwezo wa mtu kujitawala unaweza ukakinzana na upendo wake kwa mwenza wake, hivyo kuleta hali ya kutoridhika kwa mwenzi wake, kitu ambacho kinapunguza  au pengine hata kuondoa raha ya mahusiano. 
Mfano utakuta kwa kufuata makundi ya marafiki aliyonayo, mwanaume anakuwa mlevi wa kupindukia,  na kujikuta akiingia katika anasa na maamuzi mengine yasiyo mazuri kwa mpenzi wake na familia kwa ujumla. Hata hivyo mwanaume huyo huyo ukimuuliza kama anampenda mke wake au la, atakujibu anampenda sana. Tatizo nini ? Utajibiwa, ni pombe tuu ndio mmemtawala, na kwamba jamaa ana ‘kampani’ mbaya.

5. Maana isiyo sahihi ya upendo: Kuna wengi wanaodai wanao upendo lakini kiukweli walichonacho sio upendo bali ni tamaa au matakwa ya kuhitaji kutimiziwa mambo fulani. 
Maana halisi ya upendo sio vile unavyotaka fulani akufanyie mambo au jambo fulani, upendo sio vile unavyojisikia baada ya fulani kukutendea jambo uliloliona jema kwako, upendo sio vile fulani anavyokufanya ujisikie kwa sababu ya sura yake au umbo lake, BALI, upendo ni utayari wako wewe kufanya mambo yanayompendeza mwingine, kuwa tayari kuona mwingine ana furaha juu yako.  
 Kwa maana rahisi , upendo si jambo linalokuhusu wewe unajisikiaje, bali ni vile unavyotaka mwingine ajisikie.
Kwa maana nyingine, utatimiza vema upendo wako kwa kujitahidi kumfahamu mwenza wako, kutimiza yale anayohitaji (ili awe na furaha) sio kutimiza yale unayotaka wewe kwa makusudio yako binafsi. Upendo unahitaji kumheshimu mwenza wako, kumsikiliza, kumfanya akuamini, na aendelee kukuamini.
Pamoja na kuwa hisia za kimwili (chemistry) ni muhimu sana katika kujenga mahusiano yenu,  hisia za kimwili zisichanganywe na upendo. 
Kwakuwa fulani amekuvutia kimwili haina maana kuwa basi unampenda mtu huyo. 
Kufanya tendo la ndoa, sio lazima iwe ndio ishara ya uwepo wa upendo katika yenu, kwani wapo hata wanaofanya tendo la ndoa kama biashara.

Hitimisho
Mahusiano hususani mahusiano ya kimapenzi yanatutaka tuwe waajibikaji kwa wenzetu, na kwetu wenyewe. Kuwajibika kwa wenzetu ni pale tunapojifunza vya kutosha tabia,  na yale yanayompendeza na yasiyompendeza mwenza wetu. Wakati tunawajibika kwetu wenyewe kwa kujifunza kuhusu mapungufu yetu, na kujituma kujirekebisha. Mapenzi yanaleta majukumu, na bila kutambua na kutimiza majukumu husika, mara nyingi mapenzi yatageuka kuwa karaha, badala ya furaha.
 

Source: http://samsasali.blogsport.com/2013/04/sababu-5-kwanini-upendo hautoshi_29.html