SABABU 5 KWANINI UPENDO HAUTOSHI KUJENGA MAHUSIANO BORA
Ukisoma
kwa kutafakari makala hii utagundua kuwa kuweza kujifahamu sisi wenyewe
vema, kuweza kujitawala sisi wenyewe, na pia kuweza ‘kuwasoma’ vema
wenzi wetu , ni mambo ya msingi sana ili upendo tulionao uweze kudumisha
mahusiano. Msisitizo ni kwamba, pamoja na ukweli kuwa upendo ni kitu
cha muhimu katika mahusiano, makala hii inaeleza kuwa kutegemea upendo pekee kama nguzo kuu ya mahusiano bora kunaweza kuwa jambo la hatari kwa mahusiano, kwa sababu zifuatazo:-
1. Binadamu ni kiumbe huru: Ni
muhimu kukumbuka hili hasa kama unadhani kwakuwa unampenda fulani na
umemuonyesha mapenzi yako yote basi hicho ni kama kifungo kwake kuwa
hatoweza kutoka katika penzi lenu. Kwa asili binadamu ni huru, na
anaweza kuamua kuutumia uhuru wake kufanya maamuzi mengine yoyote
tofauti na unavyofikiri ni lazima afanye. Kwa kuwa pia ni mbinafsi,
basi kama upendo wako wote kwake hauendani na yale anayotazamia ,
unaweza kukuta ameshindwa kukaa katika penzi , ambalo kwa watu wengi
wanaona kuwa ni penzi zito.
2. Binadamu ni mbinafsi kwa asili: Binadamu
kwa asili huangalia maslahi yake kwanza kabla ya kuangalia ya mwingine.
Mfano dhahiri wa ubinafsi huu ni pale inapotokea ajali , mara nyingi
mtu huwaza kujiokoa mwenyewe kwanza kabla ya kufikiria wa karibu yake.
Tumesikia habari za mama mzazi kuacha kitoto kichanga ndani wakati moto
ukiendelea na yeye kutoka nje. Kuna habari pia za mama kumtumia mtoto
wake kama ‘kifaa’ cha kuvunjia kioo cha gari , ili aweze kujiokoa, pale
ambapo ajali ilitokea. Hivyo upendo tuu pekee hautoshi kumfanya mtu
aendelee kukaa katika ndoa au mahusiano kabla ya ndoa (uchumba), ni
muhimu yawepo mambo mengine yenye manufaa kwa mtu husika.
3. Binadamu ana mahitaji mengi na yasiyo na kikomo: Mwenza
wako ana mahitaji mengi na yanaongezeka na kubadilika siku hadi siku
kutegemeana na mabadiliko mbalimbali kama vile hali ya hewa, aina ya
kazi, watu anaokutana nao, mabadiliko ya teknolojia, mabadiliko ya
kiuchumi n.k. Upendo wenu, hausimamishi mahitaji haya yasitokee, na
kwamba upendo pekee hauwezi kuwa jibu la kutimiza mahitaji hayo.
Inahitajika bidii katika kujituma kujiletea kipato, kuwa na mawasiliano
bora kati yenu, kutambua mabadiliko na kuchukua hatua kabla mabadiliko
hayajawabidilisha, na zaidi sana muweze kuwa na utamaduni wa kupanga
mambo pamoja na kuwa waaminifu katika kutimiza yale mnayopanga.
Chukulia
mfano, wa wanandoa walioishi vema kwa miaka 5 ya ndoa, halafu ndoa
ikaanza kulemaa kwa kuwa mmoja wao anaona hakuna uwajibikaji katika
kumsaidia mwengine kujiendeleza kielimu, kibiashara, au kutimiza ndoto
nyingine ambayo mwanandoa amekuwa nayo.
4. Binadamu wengi wanashindwa kujitawala: Uwezo
wa mtu kujitawala unaweza ukakinzana na upendo wake kwa mwenza wake,
hivyo kuleta hali ya kutoridhika kwa mwenzi wake, kitu ambacho
kinapunguza au pengine hata kuondoa raha ya mahusiano.
Mfano
utakuta kwa kufuata makundi ya marafiki aliyonayo, mwanaume anakuwa
mlevi wa kupindukia, na kujikuta akiingia katika anasa na maamuzi
mengine yasiyo mazuri kwa mpenzi wake na familia kwa ujumla. Hata hivyo
mwanaume huyo huyo ukimuuliza kama anampenda mke wake au la, atakujibu
anampenda sana. Tatizo nini ? Utajibiwa, ni pombe tuu ndio mmemtawala,
na kwamba jamaa ana ‘kampani’ mbaya.
5. Maana isiyo sahihi ya upendo: Kuna
wengi wanaodai wanao upendo lakini kiukweli walichonacho sio upendo
bali ni tamaa au matakwa ya kuhitaji kutimiziwa mambo fulani.
Maana
halisi ya upendo sio vile unavyotaka fulani akufanyie mambo au jambo
fulani, upendo sio vile unavyojisikia baada ya fulani kukutendea jambo
uliloliona jema kwako, upendo sio vile fulani anavyokufanya ujisikie kwa
sababu ya sura yake au umbo lake, BALI, upendo ni utayari wako wewe
kufanya mambo yanayompendeza mwingine, kuwa tayari kuona mwingine ana
furaha juu yako.
Kwa maana rahisi , upendo si jambo linalokuhusu wewe unajisikiaje, bali ni vile unavyotaka mwingine ajisikie.
Kwa
maana nyingine, utatimiza vema upendo wako kwa kujitahidi kumfahamu
mwenza wako, kutimiza yale anayohitaji (ili awe na furaha) sio kutimiza
yale unayotaka wewe kwa makusudio yako binafsi. Upendo unahitaji
kumheshimu mwenza wako, kumsikiliza, kumfanya akuamini, na aendelee
kukuamini.
Pamoja
na kuwa hisia za kimwili (chemistry) ni muhimu sana katika kujenga
mahusiano yenu, hisia za kimwili zisichanganywe na upendo.
Kwakuwa fulani amekuvutia kimwili haina maana kuwa basi unampenda mtu huyo.
Kufanya
tendo la ndoa, sio lazima iwe ndio ishara ya uwepo wa upendo katika
yenu, kwani wapo hata wanaofanya tendo la ndoa kama biashara.
Hitimisho
Mahusiano
hususani mahusiano ya kimapenzi yanatutaka tuwe waajibikaji kwa
wenzetu, na kwetu wenyewe. Kuwajibika kwa wenzetu ni pale tunapojifunza
vya kutosha tabia, na yale yanayompendeza na yasiyompendeza mwenza
wetu. Wakati tunawajibika kwetu wenyewe kwa kujifunza kuhusu mapungufu
yetu, na kujituma kujirekebisha. Mapenzi yanaleta majukumu, na bila
kutambua na kutimiza majukumu husika, mara nyingi mapenzi yatageuka kuwa
karaha, badala ya furaha.
Source: http://samsasali.blogsport.com/2013/04/sababu-5-kwanini-upendo hautoshi_29.html
