Monday, 24 June 2013

ZIJUE KAZI ZA ROHO MTAKATIFU KWETU WANADAMU



ROHO MTAKATIFU,MTOA UTAKATIFU
Katika somo la kwanza katika mfululizo wa masomo haya yanayohusu Roho Mtakatifu,Tulijifunza kwamba Roho Mtakatifu,ni mtakatifu,hivyo anakuwepo na kudumu mahali palipo na utakatifu tu.Tukiwana maisha ya uchafu,yaani dhambi;humfanya Roho Mtakatifu akose makao kwetu,na hivyo hawezi kuwepo kwetu.Kama alikuwepo mwanzo kwetu,huondoka (1Samweli 16:14;
Zaburi 51:4,10-11).Sasa swali linakuja,tunawezaje kuwa watakatifu katika maisha yetu ili Roho Mtakatifu afanye makao
kwetu?Jibu ni kwamba,Roho Mtakatifu ,ndiye huyohuyo anayetoa utakatifu tunaouhitaji.Sasa tunamwangalia Roho
Mtakatifu kama Mtoa Utakatifu,kwa kutafakari kazi yake hiyo katika vipengere vitano:-

1. ROHO MTAKATIFU,ROHO ATUPAYE KUZALIWA MARA YA PILI 

Hatupaswi kamwe kudanganyika kwamba utakatifu siyo duniani ni mbinguni,Maandiko yanaeleza waziwazi
kwamba watakatifu walioko duniani ndiyo anaopendezwa nao Mungu(Zaburi 16:3).Hatupaswi pia
kudanganyika kwamba tunaweza kufanya dhambi hapa duniani,halafu tukasalimika baada ya kufa,kutokana
na misa ya wafu n.k(1Wakorintho 6:9-10;Waefeso 5:5-7;Wagalatia 6:7;Waebrania 9:27;IYohana 5:16;Kumbukumbu 10:17) la maana hapa ni kufahamu ni jinsi gani tunavyoweza kuwa na ushindi dhidi ya
dhambi hapa duniani,na kuokoka kutupwa motoni,maana bila shaka tunatakiwa kuokoka tukiwa hapahapa
duniani (Luka 19:8-10);Tito 3:3-4)Tunawezaje kuwa na ushindi dhidi ya dhambi?Ni kwa kuzaliwa mara
ya pili,kwa Roho Mtakatifu(Yohana 3:3-10;Tito 3:3-5)Yesu Kristo,alijaribiwa sawasawa na sisi lakini
hakutenda dhambi(Waebrania 4:14-15)Ni nini siri ya ushindi wake huo?Ni kwa sababu alizaliwa kwa
Roho Mtakatifu,yaani alizaliwa tofauti na kawaida ya kimwili ya mume na mke.Sisi nasi tunapotubu dhambi
zetu kwa kumaanisha kuziacha,tunapata rehema hii kwa imani tu(Mithali 28:13)Tunazaliwa mara ya pili
katika ulimwengu wa roho,na hivyo kuwa na uwezo wa kushinda dhambi kwa muujiza mkubwa.Katika
hali ya kawaida ya jinsi tulivyozaliwa kimwili,kamwe hatuwezi kushinda dhambi.Ni mpaka tufanyike viumbe
vipya kwa Roho Mtakatifu.Mwambie Roho Mtakatifu kwamba unataka kuzaliwa mara ya pili,naye atafanya.

2. ROHO MTAKATIFU ROHO AWAFUFUAYE WATU WALIOKUFA KIROHO
 
Kurudi nyuma na kuacha wokovu kunaitwa pia kufa kiroho(Ufunuo 3:1;Waefeso 2:1).Kwa kila aliyerudi nyuma
na kuacha wokovu,hii ni saa ya kuamka usingizini na kuanza upya(Warumi 13:11-12).Lakini,je,inawezekana
kuanza upya tena katika hali hii?Ndiyo,kwa msaada wa Roho Mtakatifu.Hii ni kazi yake nyingine.Roho Mtakatifu
ndiye aliyemfufua Yesu,alipokufa(Warumi 8:11).Kwa jinsi hiyo hiyo,Roho Mtakatifu anaweza kutufufua kiroho
na kutupa uhai tena wa kiroho(Waefeso 2:1,4-6).Mwambie Roho Mtakatifu kwamba unataka kufufuliwa kiroho,
naye atafanya.

3. ROHO MTAKATIFU, ROHO AWATIAYE UZIMA WATU
 
Kabla ya kufa kiroho,hutangulia kuzimia kiroho.Shetani hutupeleka hatua kwa hatua,kama upepo katika tairi
unavyotolewa kidogo kidogo kutokana na pancha ndogo.Tukizimia kiroho,upendo wa kwanza unatoweka.
Ingawa bado hatujafikia hali ya kufanya dhambi za uzinzi,uasherati,ulevi n.k kama mataifa,hata hivyo,mambo
ya rohoni yanakuwa hayana mvuto kwetu kama mwanzo.Kuomba,kushuhudia,kuhudhuria ibada n.k,yanakuwa
mzigo kwetu.Tunaanza kuvutwa zaidi na mambo ya dunia.Katika hali hii tunahitaji nguvu mpya,uzima mpya
(Isaya 40:28-31).Anayefanya kazi hii pia ni Roho Mtakatifu,Roho wa uzima(Warumi 8:2).Pepo wa udhaifu
wanatolewa kwa Roho wa Mungu(Mathayo12:28),na vivyo hivyo udhaifu wetu kiroho unatolewa na
Roho wa Mungu.Je umezimia kiroho,Mwambie Roho Mtakatifu akuzindue,naye atafanya.