WANAUME MBEYA WAJITOKEZA KWA WINGI KUPIMA KISUKARI NA SHINIKIZO LA DAMU KUFUATIA BIMA YA AFYA KUPIMA BURE UWANJA WA SOKOINE IKIWA NI MAADHIMISHO YA MEI MOSI INAYOFANYIKA KITAIFA MKOANI MBEYA HUKU WANAWAKE WAKITAKA KUPIMA UKIMWI
BAADHI
YA MAAFISA WA MFUKO WA BIMA YA AFYA MKOANI MBEYA WAKIWA KWENYE BANDA LA
UPIMAJI WA AFYA BURE, HUDUMA INAYOTOLEWA NA MFUKO HUO AMBAPO BAADA YA
KUPIMWA WANANCHI HUPEWA USHAURI.
Na Mgalula Joseph, Mbeya
WANAUME mkoani
Mbeya wengi wamejitokeza kupima magonjwa ya Kisukari na shinikizo la damu huku
wanawake wakijitokeza kwa wingi kupima VVU.
Hali hiyo
imebainika katika banda la mfuko wa taifa wa bima ya afya(NHIF)lililopo katika
uwanja wa Sokoine ambako mfuko huo unatoa huduma ya upimaji bure ikiwa ni
kuazimisha siku kuu ya wafanya kazi (Mei mosi) inayofanyika kitaifa mkoani hapa
na mgeni rasmi ni Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza
na Mtandao wa www.kalulunga.blogspot.com afisa uhakiki na ubora wa mfuko huo, Dr. Lucas Gama,
alisema kuwa wananchi wengi wameendelea kujitokeza kupima afya zao tangu jana
wakiwemo wanawake na wanaume hasa vijana.
‘’Wanajitokeza
kwa wingi, lakini wanawake wengi wanaokuja wanasema wanataka kupima Ukimwi
wakati wanaume wanaokuja wanauliza tunapima nini na tukiwaambia tunapima
Kisukari na shinikizo la damu wanaongezeka kuja kupima’’ anasema Dr. Gama.
Alisema kuwa
imejengeka tabia kwa baadhi ya wananchi kuona kuwa Ukimwi ni ugonjwa hatara
wakati ugonjwa huo hauuwi haraka tofauti na magonjwa kama kisukari na shinikizo
la damu(BP).
‘’Magonjwa
haya ni magonjwa hatari na yanaua haraka kuliko Ukimwi, jana tumewapata
wagonjwa watatu ambao wana sukari 200 jambo ambalo ni hatari sana na tumewapa
ushauri na hapo utagundua kuwa watu wanatembea na majeneza’’ alisema Dr. Gama.
Alifafanua
kuhusu magonjwa hayo kuwa shirika la afya duniani(WHO), linasema kuwa Sukari na
shinikizo la damu ni viashiria vya afya ya mtu, ambapo sukari ikiwa 7 kwenda
chini ni sukari ya kawaida ila kwenda juu mtu akiwa hajala ni hatari.
Kwa upande wake
afisa wa NHIF mkoa wa Mbeya Reginald Kileo, alisema kuwa mfuko huo umeona
umuhimu wa kutoa huduma hiyo bure ili
wananchi waweze kuwa na mazoea ya kupima afya zao.
‘’Watu
wanatembea na makaburi lakini hawajui, hivyo ni muhimu serikali ikaendelea
kutoa elimu kwa wananchi kujitokeza kupima afya zao na iwe bure’’ alisema
Kileo.
Mwananchi
Agness Mojo mkazi wa Soweto na Jackson Matengula mkazi wa Uyole ambao ni baadhi
ya waliojitokeza kupima afya zao walisema kuwa wanashindwa kupima afya zao
hospitali kutokana na kutozwa fedha huku mapokezi yakiwa hayaridhishi.
Upimaji huo
wa afya bure, unaishia kesho siku ya Mei mosi katika viwanja vya Sokoine kupitia
mfuko huo wa taifa wa bima ya afya.
