SURA YA
NNE
KUSUDI KUU NA LA KWANZA
Katika sura iliyopita, tumegundua sababu
inayomfanya Mungu kupenda sana sifa na ibada,; na sit u kupenda, bali pia
kutaka sana sifa na ibada. Huko mbeleni, tutaona hata jinsi anavyoagiza kwamba,
watu wote wamsifu. Hiyo sasa imegeuka kuwa amri! Kumsifu Bwana ni agizo!
Tutaiangalia hiyo baad ya muda mchache. Lakini katika sura iliyopita,
tumeshaelewa kwanini Mungu anahitaji sifa na kwanini anataka sifa na ukuzo.
Tumegundua kwamba, mungu anataka hvyo vyote kwasababu yeye anaishi katika sifa
na tukuzo za watu wake. Na tumeona jinsi Mungu alivyo very very serious kuhusu
kupata hayo sifa na utukufu wake.
Yaani katika hili, Mungu yuko very serious, wala
hatanii na wala hataki mchezo, kuhusu ibada. Nenda kamuulize mwanamke mmoja
anaiwa Mikali, mke wa mfalme Daudi,
atakueleza ukali wa Mungu juu ya sifa na ibada. Hapo ndio utaelewa vizuri nini
maana ya Mungu kutopenda utani kuhusu maswala haya ya kusifiwa na ibada. Maana
Biblia inatuambia kwamba, Mfalme Daudi alipokuwa akimsifu Mungu na kucheza
mbele za Mungu kwa muziki mzuri, mbele ya watu wengi, Daudi alicheza sana mpaka
nguo zake zikaanguka, akabaki kifua wazi. Piga picha, Mfalme alibaki kifua wazi
mbele ya kadamnasi, kwasababu ya kucheza nyimbo za kumsifu Mungu.
Basi Biblia inasema, mke wa Daudi alikuwa
ghorofani, akiangalia ile ibada. Na moyoni mwake, alikereka sana kumwona mume
wake anavyocheza na kuangusha mavazi yake ya kifalme, hata kubaki karibu na
‘uchi’ mbele za watu. Hicho kilimkera sana Mikali binti wa Sauli, ambaye alikuwa
mke wa Mfalme Daudi. Na Biblia inasema kwamba, huyu mwanamke, alimdharau sana
na kumdhihaki sana mume wake kwa kile kitendo cha kucheza kwa ajili ya Mungu,
hata kuangusha nguo zake. Basi Mfalme Daudi alipomaliza ibada, akapanda
ghorofani kwake ili kuoga, ndipo alipokutana na mke wake aliyekuja sura na
kuvua midomo yake pembeni kwa dharau, huku akimpiga jicho mume wake, kuanzia
juu mpaka chini, kwa dharau kubwa kabisa.
Biblia inasema, huyu mama alianza kumporomoshea
mume wake maneno ya dharau na aibu, eti kwa vile alivyoonyesha kifua chake na
mapaja yake mbele za watu, hasa mabinti waliokuwepo pale katika uwanja au katika
ua wa hekalu. Biblia inasema, huyu mama alidiriki hata kumwita mume wake ‘baladhuli
mkubwa’ yaani pumbavu, punguani au mshenzi. Duh! Kweli huyu mwanamke,
alikereka. Lakini Biblia inasema kwamba, Mfalme Daudi, hakutetereka.
Bali alimwambia mke wake kwamba, yeye ataendelea kumsifu Mungu hata kama watu
hawatamwelewa.
Sasa, nimekusimulia hii habari ya kweli kabisa,
ili tu kukuonyesha jinsi ambavyo, Mungu huwa hataki utani wala mzaha wala
mchezo katika sifa zake. Yaani utaona jinsi ambavyo, Mungu hataki uzembe wala
mchezo wa aina yoyote, inapokuja katika maswala ya kumsifu na kumtukuza yeye.
Ninaomba uisome mwenyewe hii habari, ili upate picha yako binafsi kadri Mungu
atakavyokusaidia kuielewa. Lakini katika habari hii, Mungu alikuwa mkali sana.
Kwasababu kabla hata mazungumzo yao hayajaisha, Mungu alikuwa ameshuka kwa
hasira. Maana Biblia ibasema kwamba, Mungu alimfunga tumbo Yule mama, tangu
siku ile aliyoleta madharau yake kwa Daudi ambaye amekuwa chombo cha Bwana
kiteule kwa sifa na ibada.
Biblia inasema
kwamba, Mikali alikufa bila kupata mtoto, kwasababu ya kujaribu kumkatisha tama
Daudi. Mimi najaribu kupiga picha ya kibinadamu, jinsi Mungu alimkaripia yule
mama. Japo Biblia haisemi, lakini mimi nafikiri tu kibinadamu, jinsi Mungu
alivyoteremka kwa hasira kali kabisa, akitaka kumzaba kibao huyu mwanamke,
kwasababu ya maneno yake ya kukatisha tama na matusi yake dhidi ya chombo cha Mungu,
yaani Daudi. Yaani ni kama vile, feni zote zimezimika, halafu kuna feni moja tu
imabaki ndiyo inayofanya kazi, halafu anakuja mtu mmoja mjinga, asiyejua umuhimu wa feni, na kuanza kuichokonoa akitaka na
yenyewe eti izimike kama zingine.
Hebu piga picha
jinsi baba mwenye nyumba, anayeishi kwa hewa itokanayo na feni ile, jinsi
ambavyo angesimama kutoka kwenye kochi alilokuwa amejipumzisha, na kumwendea mjinga huyu kwa hasira, akitaka kumzaba
makofi, kwa jinsi anayochezea feni yake tukufu. Japo Biblia haisemi, lakini
mimi najaribu kupiga tu picha ya kibinadamu, jinsi Mungu alivyomteremkia Mikali
kwa hasira, akitaka kumzaba makofi, kwasababu ya maneno yake ya kedehi na
matusi, kwa mtumishi wa Mungu Daudi; ambaye kwa wakati huo, ndiye alikuwa kama
vile ndiye feni pekee ya Mungu, iliyokuwa inampa Mungu hewa
saaaaafi wakati wa joto, hewa hiyo inaitwa, sifa
na ibada.
Mimi naamini,
Mungu alisimamisha au alizuia kofi lake, sentimita chache tu kutoka shavuni kwa
Mikali. Mimi naamin kwamba, Mungu alijua, nikimtandika mwanamke huyu kofi,
lazima atakufa; na akifa, hapo nitakuwa nimeleta msiba na huzuni nyumbani kwa
mwanangu Daudi. No! ngoja niache. Ndiyo maana Mungu alizuia kofi lake,
sentimita chache tu kabla halijampata Mikali shavuni kwake. Ni kwasababu ya Daudi
tu, rafiki wa Mungu, ndiyo maana Mungu alimsamehe Mikali. Yaani isingekuwa
Daudi, mimi naamini kwamba, Mungu angemkaanga huyu mwanamke, kwa radi na moto
wa mbinguni (Soma 2Wafalme 1:10-14, uone mfano wake).
Kwahiyo, mimi
naamini kabisa ya kwamba, Mikali alipona kifo, ni kwasababu tu ya Daudi, rafiki
wa Mungu. hakika asingekuwa mke wa Daudi, mimi naamini kwamba, Mungu
angeshamkaanga kabla hata hajamaliza makebehi na matusi yake. Yaani nakwambia,
kwa radi na moto wa mbinguni vingemteremkia huyu mama. Lakini Mungu akayatunza
maisha yake, japo alikuja kwa hasira na nguvu, lakini Mungu aliyatunza maisha
yake, kwasababu ya daudi rafiki yake. Lakini pamoja na hayo, Biblia iansema
kwamba, Mungu hakumwacha hivi hivi tu bila angalau kumfinya kidogo. Lakini kabla
Mungu hajageuza kurudi mbinguni, Biblia inasema kwamba, Mungu alimfinya huyu
mwanamke tumbo lake.
Katika mawazo
yangu, ninaweza kupiga picha Mungu akimwambia Mikali kwamba, ‘ni kwasababu tu
ya rafiki yangu Daudi nimezuia mkono wangu usitue juu yako; lakini pamoja na
hayo, siwe ondoka hapa nikuache hivi hivi bila alama yoyote. Kuishi, utaendelea
kuishi, hiyo nimekupa; lakini kuanzia sasa (Mungu akamshika tumbo na kumfinya
huku akiendelea kusema) … lakini kuanzia sasa, hautashika mimba tena! Mwone
kwanza! Na usirudie kuwakebehi na kuwatukana watu ambao ni kama feni au
air-condition kwangu. Tena utasa wako na uwe fundisho kwa wenzako wote
wanowadharau wale ambao huwa wananisifu na kucheza mbele zangu ibadani. Nenda
ukawape salamu zangu.’ Ndipo Mungu akaondoka zake.
Jamani, ngoja
niwe wazi mapema, kabla haujagundua mwenyewe. Ukienda kuisoma hii habari katika
Biblia, hautaikuta kama hivi ninavyosimulia. Mimi nimetumia tu lugha nyingi ya
kimawazo inayofanana na uhalisia wa maisha ya kibinadamu, jinsi ambavyo sisi
kama binadamu, huwa tunakarika na kuadhibu watu. Ila ukienda kuisoma mwenyewe,
utaelewa jinsi mawazo yangu ambavyo hayako mbali na vile ilivyoelezewa katika
Biblia. Mimi ni mwalimu, kwahiyo ninajaribu tu kukutengenezea picha ya uhalisia
wa dhana au concepts hizi
ninazokufundisha na ninazokusomea katika maandiko matakatifu. Kwahiyo, usiache
kwenda kufungua Biblia mwenyewe. Habari hii imeandikwa katika Kitabu cha Pili cha Samweli, Sura ya Sita
yote. Japo nimekuchanganyia lugha ya picha, na nadhani imekusaidi kuelewa
jinsi ambavyo Mungu ni mkali sana kuhusu sifa zake. Kama tulivyoona kule
mwanzoni kwamba, Mungu yuko very very serious, kuhusu sifa na ibada. Yaani
hataki utani wala mchezo. Na tumesoma
jinsi Mungu alivyokuwa mkali kwa Mikali mke wa Daudi, na jinsi alivyomfurikia,
yaani jinsi alivyomjia kwa nguvu na kwa jazba na kwa hasira kali kama mafuriko.
Kwahiyo, kuhusu sifa, Mungu ni mkali sana. Hii ni kwasababu, Mungu anapenda
sana sifa na anataka sana sifa na tukuzo.
Pengine wewe
umeona mtu kufungwa tumbo na Mungu kwasababu ya kebehi juu ya ibada, ni kitu
kikubwa sana. Lakini ukisoma kuanzia mstari wa 1 hadi wa11, wa kitabu hiki (2
Samweli 1:1-11), tunaona jinsi ambavyo Mungu alikuwa tayari hata kuuwa mtu, eti
tu kwasababu, taratibu zake za ibada, hazikufuatawa. Kufunga tumbo ni kitu
kidogo sana ukilinganisha na kuuwawa kwa mtu. Mungu ni mkali sana inapofika
katika maswala ya kusifiwa na kuabudiwa. Biblia inasema kwamba, Daudi alilibeba
sanduku la Bwana juu ya gari la kuvutwa na ngómbe, badala ya kubebwa na
makuhani. Biblia inasema, Mungu alimwagiza Musa kusema kwamba, sanduku hilo la
agano, litabebwa na makuhani na walawi peke yao.
Lakini katika
habari hii, Biblia inasema kwamba, Mfalme Daudi, hakufanya hivyo, bali
aliliweka sanduku la Bwana juu ya gari la kukokotwa na ngómbe. Hiyo iliifanya
ibada yao yote kuwa makeleele tu mbele za Mungu. yaani, Mungu aliikataa
kwasababu maagizo yake hayakufuatawa. Pamoja na nyimbo nzuri na kucheza sana,
lakini Mungu aliikataa ile ibada. Na ili kuikatisha ile ibada, Mungu
akamsababisha ngómbe mmoja ajikwae au ateguke, ili gari lililobeba sanduku
liiname, na sanduku liwe kama linateleza ili kuanguka. Ndipo mtu mmoja katika
msafara huo, aliyeitwa Uza, alipolikimbilia ili kulishika sanduku la Agano, na
kliokoa kwa nia njema kabisa; lakini kwasabubu yeye si kuhani, Mungu
akamfurikisha na kumtandika mara moja. Biblia inasema, Uza akafa pale pale.
Hiyo inakuonyesha jinsi Mungu alivyo mkali kuhusu sifa na ibada yake.
Jamani, hivi ndivyo
ambavyo Mungu wetu alivyo; Mungu yuko very very serious kuhusu kusifiwa na kuabudiwa. Sasa, kwa
mfano huo huo, ni muhimu uelewe kwamba, viumbe wote sisi, tumeumbwa na Mungu
duniani, ili tuwe kwake kama vyombo maalum vya kumsifu na kumwabudu yeye Mungu. Kusifu na kuabudu kunatupa sababu na
maana ya sisi viumbe kuishi. Na ndio
maana Daudi alipoelewa ufunuo huu, akajiambia mwenyewe, kusema “… Ee
nafsi yangu, umsifu Bwana”. Halafu katika mstari wa pili, Daudi
anatuambia na sisi wengine kwamba;
“Nitamsifu Bwana, muda ninaoishi, nitamwimbia
Mungu
wangu ningali ni hai” (Zaburi 146: 1-2).”
Ufunuo
wa Mfalme Daudi.
Na ndio maana,
Roho Mtakatifu alipompa Mfalme Daudi ufunuo huu; Kwamba viumbe wote ni vyombo
maalum vilivyoumbwa kumsifu na kumwabudu Mungu, Daudi akaandika tena waraka
maalum au wimbo maalum kwa viumbe wote, ili kuwaamuru na kuwakumbusha, watenge
muda maalum wa kumsifu na kumwabudu Mungu. Mfalme Daudi akaandika waraka huo au
wimbo huo katika Zaburi 148.
Zaburi 148 inasema hivi; Tena
akawaanzia viumbe wa huko huko mbinguni, akasema;
“Halleluyah.
Msifuni Bwana kutoka mbinguni; msifuni katika mahali palipo juu. Msifuni, enyi
malaika wake wote; Msifuni, majeshi yake yote.
Halafu akatelemka kidogo hapa duniani, lakini akaanzia
kwa viumbe wa angani, akawapa na wao maneno yao, akasema;
Msifuni
jua na mwezi; Msifuni, nyota zote zenye mwanga. Msifuni, enyi mbingu za mbingu;
Nanyi maji mlioko juu ya mbingu (mawingu)msifuni, na vilisifu jina la Bwana,
kwa maana aliamuru, vikaumbwa. Amevithibitisha hata milele na milele, ametoa
amri na haitapita.
Halafu akatelemka zaidi huku duniani, kwa viumbe wa
ardhini, na wao wakapewa maneno yao, akawaambia akisema;
Msifuni
Bwana kutoka nchi, Enyi nyangumi na vilindi vyote. Moto na mvua ya mawe (yaani
vitu vigumu-yabisi- na vimiminika), theluji na mvuke (yaani vitu vya baridi
zaidi na vitu vya moto zaidi, vyote vilisifu Jina la Bwana) pia akasema na Upepo wa dhoruba ulitendao neno lake (Vyote vilisifu Jina la Bwana);
halafu akaongea na Milima na vilima
vyote (yaani mikubwa na midogo, vyote vlisifu Jina lake); halafu akasema
na, Miti yenye matunda na mierezi yote
(yaani inaytoa matunda na ile isiyotoa matunda, yote ilisifu Jina lake);
kisha akasema na, Hayawani, na wanyama
wafugwao (yaani wanyama wasiofugwa na wanaofugwa, wote walisifu Jina la Bwana);
halafu akaongea na, vyote vitambaavyo na
ndege wenye mbawa (yaani wale wanaoruka na wale wanaotambaa, wote walisifu Jina
la Bwana);
Kisha akaja kwa binadamu, na sisi, akatupa maneno yetu, aksema;
Wafalme
wa dunia na watu wote (yaani wafalme na wasio wafalme, wote walisifu Jina la
Bwana); kisha akasema, wakuu na makadhi wote wa dunia (wote
walisifu Jina la Bwana); halafu akasema, vijana waume, na wanawali (yaani wakiume na wakike, wote walisifu jina
la Bwana); halafu akasema, wazee
wote, na watoto pia; Na walisifu jina la Bwana, Maana jina lake peke yake
limetukuka; Adhama yake i juu ya nchi na mbingu …”
Kwa kuisoma
mistari hii ya waraka wa Mfalme Daudi kwa viumbe vyote, tunapata kuelewa
kwamba, viumbe wote tunaishi ili tumpe Mungu sifa na ibada. Hili ndilo kusudi
la kwanza na la muhimu zaidi kwa viumbe wake, la kutufanya sisi viumbe tuwepo
duniani. Hivyo basi, maisha yako yatakuwa na maana zaidi, na thamani zaidi, mbele
za Mungu, kama wewe utakuwa mwaminifu kutimiza makusudi ya kuumbwa kwako, yaani
kumsifu
na kumwabudu Mungu. Mungu anataka kusifiwa, tena Mungu anataka
kuabudiwa.
Kwa waraka huu
wa Mfalme Daudi, utagundua kwamba, Kusifu
na Kuabudu ni Amri! Ni Maagizo! Na
Sio Ombi! Kama Zaburi hii inavyosema katika mstari wa 5 na wa 6, inasema;
Viumbe vyote vilisifu jina la Bwana, kwa
maana aliamuru hivyo, hata vikaumbwa;
tena Amevithibitisha hata milele na milele, halafu Ametoa amri na haitapita!!!
Hivyo basi,
ikiwa tunapumua, basi ujue tunapumua ili kumsifu Mungu. Mioyo yetu inadunda,
bila kuwekewa betrii au charge ya umeme, ili tuwe vyombo vizuri vya ibada.
Mpendwa, uhai wetu na maisha yetu, ni kwa ajili ya kumsifu na kumwabudu Mungu
kwanza. Kwahiyo, maisha yako na uhai wako, yatakuwa na thamani yake na umuhimu
wake, pale tu, utakapolitimiza hili kusudi la kumsifu na kumwabudu Mungu. Hivyo basi, kwa kusema hivi, ina maana
kwamba, kama siku nzima, yenye masaa 24, itapita, bila wewe kupata muda wa
kukaa kwa utulivu mbele za Mungu na kumpa Mungu sifa na ibada kutoka kwako,
basi ujue siku hiyo imepita kihasara mbele za Mungu.
Ngoja nirudie
nilichosema. Usisome tu kwa macho yako tu, soma pia kwa moyo wako wote kabisa!
Yaani hapa … ninamaamisha hiviiii; Hata kama wewe umetengeneza faida ya
mamilioni na mamilioni, ya shilingi au ya dollar au pesa yoyte ile katika shughuli
zako za siku hiyo, lakini kama wewe hukupata muda wa kukaa kwa utulivu mbele za
Mungu na kumpa Mungu sifa na ibada, basi ujue, katika siku hiyo, imepita kwa
hasara mbele za Mungu, katika siku hiyo, Mungu amehesabu hasara. Hii
ni kwasababu, wewe katika siku hiyo, umepata faida, ni sawa, lakini yeye aliyekuumba,
amepata hasara katika siku hiyo, kwasababu, hajapata faida ile aliyoitaka, kutoka
katika pumzi yako. Kwahiyo, Mungu amepata hasara !!!
Maisha yetu na
uhai wetu, yatakuwa na thamani yake na umuhimu wake, pale tu, tutakapolitimiza
hili kusudi la kumsifu na kumwabudu
Mungu. Ni muhimu ujue kwamba, tuna uwezo wa kupumua na kutembea na
kufanya kazi, ili tuweze kutengeneza mazingira mazuri ya kimaisha, ili hatimaye
tuwe vyombo vizuri vya kumsifu Mungu na kumwabudu. Mioyo yetu inadunda vizuri tangu
kuzaliwa, bila kuwekewa betrii au charge ya umeme, ili tuwe vyombo vizuri vya
ibada; na mapafu yetu, yanatanuka na kusinyaa, hata wakati wewe umelala fofofo,
hujijui, ili tu uwe chombo kizuri cha ibada; na damu zetu, zinakimbia vizuri
katika mishipa yake, ili tuwe vyombo vizuri vya ibada.
Maisha yetu na
uhai wetu, yatakuwa na thamani yake na umuhimu wake, pale tu, tutakapolitimiza
hili kusudi la kuumbwa kwetu, yaani kumsifu na kumwabudu Mungu. Kwa ufahamu huu wa sasa, ni lazima
tuwe na nidhamu ya kutenga muda na kutafuta muda wa kujihudhurisha mbele za Mungu kila siku, kwa
kumsifu, kumwabudu na kumshukuru Mungu, kwa wema wake, kwa Baraka zake, kwa
matendo yake ya ajabu, kwa ahadi zake, na kwa vile tu alivyo; kwa uweza wake na
tabia zake kwetu. Tunatakiwa tufanye hivi, hata Mungu aone sababu ya
kutulinda, kutupa afya, kutakasa vyakula vyetu na kutubariki kwa namna
mbalimbali. Jamani, Mungu anataka sifa na ibada!
Maisha
yetu, si yetu wenyewe, ni mali yake.
Maisha yetu, si
yetu wenyewe, bali ni mali yake yeye aliyetuumba. Ametuumba ili tuwe watoto
wake wazuri, tutakaokuwa na muda wa kukaa nay eye aliye Baba wa vyote, ili
kumsifu na kumwabudu, kwasababu, anataka kusifiwa na si hivyo tu, bali
kwakweli anastahili kusifiwa.
Kwa
mfano wa mti wa tini, katika shamba la mizabibu.
Bwana Yesu
alitoa mfano wa mtini iliokuwa umepandwa na mwenye shamba, katika shamba zuri
na la thamani sana, la mizabibu. Yesu akasema hivi;
Luka 13:6-8
6Mtu mmoja alikuwa na mtini, umepandwa katika shamba lake la
mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. 7Akamwambia
mtunzaji wa shamba la mizabibu, ‘Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta
matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu. Uukate basi, mbona hata nchi
unaiharibu? 8Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao, hata
niupalilie, niutilie samadi, nao ukizaa matunda baadaye, basi vema; laa,
usipozaa, basi uukate.
Mistari hii, ni
ya muhimu sana, kutusaidia kuelewa kusudi la kwanza na la muhimu zaidi kwa
Mungu, juu ya maisha yetu. Kwa mfano wa mtini huu, unaweza kujiona wewe kama
mti wa Mungu, uliopandwa duniani, ili kumzalia Mungu matunda mbalimbali. Hebu
fikiria juu ya habari hii tuliyoisoma; japo mti huu ulikuwa hauza matunda, kama
Bwana wake alivyotegemea, lakini pengine ulikuwa ukitoa majani mazuri tu, kwa
ajili ya kulisha sungura wa mwenye shamba.
Pamoja na
kwamba, mti huu ulikuwa hauzai matunda kama Bwana wake alivyotamani, lakini
pengine mti huu ulikuwa umechanua vyema kabisa na kutambaa vizuri juu ya
chanja, hata ukaweza kutengeneza kivuli kizuuuuuri kwa ajili ya huyu mtunzaji
wa shamba, kujipooza mwili wakati wa jua kali la mchana. Kwahiyo, pamoja na
kwamba, mti huu ulikuwa una faida zingine, mbali na kuzaa matunda kama Bwana
wake alivyokuwa akitamani, lakini hapa tunaona kwamba, mwenye shamba anaamuru
mti huu kukatwa kabisa na kutupiliwa mbali.
Yaani pamoja na
hizo faida zingine, bado mwenye shamba alikuwa hajaridhishwa na hizo faida
zingine, kwasababu, hizo zote ni za pili (yaani
secondary); lakini, sababu ya kwanza aliyoitaka huyu bwana (primary), ni matunda! Na sio majani
wala kivuli! Kwahiyo, akamwambia mtunzaji wa shamba lake, akasema; ‘Tazama,
miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu. Hebu
nataka uukate mara moja, mbona hata nchi unaiharibu? Mbolea yote hii
inakwenda bure tu! na maji yote haya yanapotea bure tu! Kata!
Ingawa
hatukuwepo na haijaandikwa popote, lakini mimi najaribu tu kufikiri kwamba, Pengine
yule mtunzaji wa shamba alimsihi sana mwenye shamba, na kusema, ‘bwana mkubwa, najua mti huu hauzai matunda
kama tunavyotamani, lakini mbona katika mti huu, tunapata kivuli kizuuuri
wakati wa jua kali? Nakusihi tusiukate mtu huu’. Lakini yule mwenye shamba
akasema, No! Sitaki, hicho kivuli
unachopata, ni secondary (yaani ni kitu cha pili) lakini kitu cha kwanza, yaani
primary, mimi hapa nataka matunda! Nukta! Nimesema ukate!
Nimesema hivii,
ingawa hatukuwepo na wala haijaandikwa popote katika Biblia, lakini mimi
najaribu tu kufikiri, Pengine yule mtunzaji wa shamba alimsihi tena mwenye
shamba, na kusema, ‘bwana mkubwa, najua mti huu hauzai matunda kama tunavyotamani, lakini
kumbuka kwamba, katika mti huu huu, ndipo tunapopata majani mazuri kwa ajili ya
wale sungura wako?! Mzee, nakusihi tusiukate mti huu’. Lakini yule bwana mkubwa akasema, ‘Nimesema
No! Hivi weweee, unajua kiswahiliiii au una matatizo ya masikio?! Nimesema
hiviiiii, sitaki kuuona mti huu shambani kwangu, Nimekataa! Nasema hiviii, kata
huu mti! Hayo majani ya sungura hayo, unayoyasema unapata kutoka katika mti
huu hayo, ni sabau ya pili, (yaani, secondary), lakini kitu cha kwanza kabisa,
nilichokuwa nakitaka kwa mti huu, (yaani primary), mimi nilitaka matunda!
Nukta! Kwahiyo nimesema hiviiii, kata kabisa mti huu, … kata!!!
Duuuh! Hii kali
sana.
Mimi nadhani,
Pengine yule mtunzaji wa shamba akamsihi tena kwa mara ya tatu, tena safari
hii, huyu mtunzaji wa shamba, akaamua kumlilia kabisa huyu bwana mkubwa, na
hata kuanguka na kumpigia magoti kabisa na akimihi sana huyu mwenye shamba,
asiukate ule mti usiozaa. Akiwa chini, kwenye mavumbi kabisa, huku machozi
yakimtoka, huyu jamaa mtunza shamba akalia akisema, ‘bwana wangu, nakuomba mzee
wangu, niko chini ya miguu yako, nimeshika miguu yako kabisa mzee, nakumba sana
bwana mzee, hebu usiukate mti huu, nakuomba sana, hebu uuache kwa mwaka huu
mmoja nao, ili niupalilie, tena niutilie na samadi zaidi kidogo, na kuumwagilia
maji zaidi kidogo, nao ukizaa matunda baadaye, basi vema; lakini laa usipozaa,
basi uukate mzee. Ndipo yule mwenye shamba, akaghairi hasira yake, na
akausamehe ule mti, kwa mwaka mmoja zaidi. Pengine utazaa matunda aliyokuwa
akitamani sana kuyapata.
Na wewe, chungulia maisha yako.
Mpendwa, hebu na
wewe chukua muda kidogo, chungulia maisha yako. Kwasababu hii habari ya Mtini
huu tuliouusoma, ambayo Bwana Yesu aliitoa, ni mfano halisi kabisa wa maisha
yako. Sikia, … Ni kweli kwamba, Mungu ameruhusu tuje duniani, si kuja kwa ajili
ya kumsifu na kumuabudu yeye tuuuu masaa yote, kama wale malaika wa mbinguni;
hapana! Si hivyo. Lakini pamoja na mambo mengi ambayo Mungu ametuleta duniani
ili kuyafanya, kama vile:- kusoma,
kulima, kufuga, kuufanya biashara, kufanya kazi za kujenga, kutengeneza vitu,
kutibu magonjwa, kufundisha na kuwapa watu elimu, kuendesha watu katika vyombo
mbalimbai vya usafiri, kushirkiana na watu katika maisha, kuoa na kuolewa,
kuzaa watoto ili kutunza vizazi na vizazi, n.k. n.k.
Lakini ningependa sana uje kwamba, mambo mengine
yooooote haya, ni namba mbili! Yaani secondary! Lakini jambo la kwanza kabisa
katika mambo yooooote haya niliyoyataja, pamoja na yale ambayo sikuyataja, jambo la kwanza kabisa maishani mwetu, ni
sisi wanadamu kuwa vyombo vizuri vya sifa na ibada kwa Mungu. Hili
ndilo la kwanza, yaani primary! Yaani la kwanza kabisa
kuliko yote. Yaani ni muhimu ujue
kwamba, tumepewa uwezo na Mungu, uwezo wa kupumua na kutembea na kufanya kazi,
ili tuweze kutengeneza mazingira mazuri ya kimaisha, ili hatimaye tuwe vyombo
vizuri vya kumsifu Mungu na kumwabudu.
Hapo mwanzo nilisema kwamba, hii mioyo yetu hii,
inadunda vizuri tangu kuzaliwa, bila kuwekewa betrii au charge ya umeme, ili
tuwe vyombo vizuri vya ibada; na mapafu yetu haya, yanatanuka na kusinyaa, hata
wakati tukiwa tumelala fofofo, bila kujitambua, lakini yupo Mungu
anayeyaendesha na kuyafanya yatanuke na kurudi, wakati wewe umelala, ili tu
uweze kuwa chombo kizuri cha kumfanyia yeye aliyekuumba, sifa na ibada; hata
damu, zinakimbia vizuri katika mishipa yake, ili tuweze kuwa vyombo vizuri vya
ibada; na huo ubongo wako huo, na unaweza kufikiri na kukokotoa mambo na kufanya
kazi vizuri, ili tu, uweze kuwa chombo kizuri cha kumsifu na kumwabudu Mungu.
Mpendwa, uhai wetu na maisha yetu, ni kwa ajili ya kumsifu na kumwabudu Mungu
kwanza.
Jambo lolote unalolifanya kama kipawa au kipaji
kutoka kwa Mungu, hilo jambo ni namba mbili. Hata kama wewe ni bosi fulani, au
mkuu fulani, au kiongozi fulani, kumbuka kwamba, hilo jambo unalokimbizana nalo
kila kukicha mpaka kukichwa, hilo jambo ni secondary (yaani ni la pili); bali
jambo la kwanza kabisa, ni wewe kuwa chombo cha kumsifu na kumwabudu Mungu.
Hata kama wewe mheshimiwa jaji au hakimu, au wewe ni mkuu wa wilaya, au wewe ni
mkuu wa mkoa, au yamkini wewe ni mheshimiwa mbunge au mheshimiwa waziri fulani
au wewe ni rais wa taifa fulani au wewe ni mfalme wa nchi fulani, leo nimetumiwa
na Mungu kukufahamisha na kukumbusha kwamba, wewe ni chombo chake cha sifa na
ibada.
Yaani kwa swala hili la kupata muda wa kwenda
mbele za Mungu, haijalishi una cheo gani duniani, Biblia inasema kwamba Mungu
ndiye Baba wa vitu vyote, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, yeye ndiye mkuu
wa wafalme wote, ndiye Mfalme wa wafalme wote na Bwana wa mabwana wote, peke
yake, anastahili kuabudiwa na kutukuzwa na viumbe wote; na sisi wote tuliobaki,
ni viumbe tu, hivyo yatupasa kumsifu na kumwabudu yeye peke yake. Kumbuka hilo
siku zote.
Haijalishi unafanya nini duniani, wewe ni chombo
cha sifa kwa Mungu. Ikiwa unafundisha au unafundishwa, ikiwa unatibu au
unapooza, ikiwa unalima au unafunga, ikiwa unanunua au kuuza au vyote, ikiwa
unasaga au unafinyanga, ikiwa unajenga au unatengeneza, iwe unaendesha au
unarusha, iwe unaimba au unapiga muziki, iwe unasuka au unashona, iwe unachora,
unapaka, unachonga, anakata, unaunga, unapika, unapamba, unacheza, unakimbia,
unaruka au unarusha, n.k; nakwambia haijalishi unafanya nini hapa duniani,
nataka kukwambia kwamba, primarily, mimi na wewe ni vyombo
vya kumsifu na kumwabudu Bwana.
Jamani, pamoja na mambo yooooooote hayo yatupasayo
kuyafanya, hayo yote ni secondary tu ndugu yangu, yaani ni
mambo ya pili kwa kipaumbele; lakini yale ya primary kabisa, yaani
yale mambo ya kwanza kabisa kwa
kipaumbele maishani mwetu, sisi wote ni vyombo vya sifa na ibada kwa Mungu wetu
aliyetuumba. Sasa, usijifanye uko bize, utaishia pabaya ndugu yangu.
Kutokana na mistari hii tuliyoisoma, mimi naamini
kabisa kwamba, kuna wakati tunapojidai kufanya sala zetu fupi zile sala
tunazosali huku tukiwa na haraka za kukimbia-kimbia na kutaka kuwahi kwenye
shughuli; mimi naamini kabisa kwamba, Mungu huwa anatushangaa sana, kabisa.
Mimi naamini kabisa kwamba, Mungu huwa anawasemesha malaika na kuwaambia
kwamba, ‘hebu mtazameni huyu, eti mwenyewe ametuliaaaa, amekazana kabisa, anajidai
kusema zile sala zake zile za chap chap; zile sala zile za kubipu.’ mmhhhh,
mimi naamini kwamba, kuna wakati Mungu anasema,
‘hivi huyu mtoto huyu, eti na yeye anataka tumlinde safarini, eti na
yeye anataka tukibariki chakula chake, eti na yeye anataka tumpe mafanikio.
Yaani yeye akiwa na matatizo na mahitaji, ndiyo anakumbuka kwamba tupo. Hivi
huyu mtotooo, tumfanyeje jamani. Hebu nipeni mawazo, kwanza ana faida gani
kwetu duniani jamani? Kwasababu, akimaliza hizo sala zake hizo za dakika mbili
tu kwa siku, hizo sala zake za kubipu, ndo hapatikani tena! Yuko biiiiiiizee,
wala hapatikani tena ibadani;
Halafu Mungu anaendelea kulalamika, anasema;
Huyu mtoto, yuko biiiiiiize kwenye shughuli zake huko, wala hakumbuki
kwamba, huo mtaji wa pumzi, na wa akili, na wa nguvu, na wa afya anayotumia, ni
mimi nimempa, tena bure, wala sijamkopesha! Lakini ndo kwanza yuko biiiiiize,
eti anadai anashughuli nyingi, eti anadai ametingwa eti, yuko very tight,
hapatikani kwenye maombi, wala hana muda wa kusoma neno langu; wala hana muda
wa kuimba nyimbo kadhaa za kunisifu na kuniabudu katika masaa yote 24
niliyompa.
Halafu Mungu anaendelea kulalamika, anasema;
Yaani katika vipande 96 vya robo saa, vilivyo ndani ya masaa 24 niliyompa
katika siku moja, yaani hawezi kunipa hata vi-4 kati ya vipande 9 nilivyompa.
Hawezi kunipa ngalau saa 1 tu kwa siku, katika mass 24 yote niliyompa!?!?
Badala yake, akijitahidi sana, anasema zile sala zake za kubipu. Tena akitoka
hapo kwenye sala zake hizo za kubipu, mpaka amekuja tena kusali, ujue amebanwa
katika tatizo au hitaji fulani, au amishiwa. Jamani, mbona hata anawamalizia
wengine hewa?’
‘Hiviii huyu mtoto, hajaambiwa kwamba, mimi Baba yake, ninajua haja zake na
mahitaji yake kabla hata hajaomba? Hiviiii, huyu mtoto, hajui kwamba, shauku ya
mimi Baba yake, ni kukaa na yeye na kuwa na muda mzuri wa ibada pamoja naye na
kumburudisha nafsi yake kwa utukufu wangu?! Hiviii, huyu mtoto? Hakuwahi
kuambiwa kwamba, na mimi Mungu Baba yake nina moyo, na sio jiwe, moyo unaotaka
kupendwa? (Kumbukumbu 6:4-9).
Halafu Mungu kutushangaa na kusema;
Hebu mwangalieni, Eti na yeye anasali kabla ya kula, eti anataka nimbarikie
chakula chake, hiviii, tumbarikie hicho chakula halafu iweje? Ili aendelee
kutimua mbio mtaani? Asipatikane katika uwepo wangu? mmhhh, laiti angejua
ninachomuwazia’.
Halafu Mungu anawauliza wenzake wa mbinguni,
‘Jamani, hebu nipeni mawazo, tumfanye nini mtoto kama huyu? Nipeni
mawazo jamani, mimi nataka kumkatilia mbali, kwasabau hebu Tazama, ni
miaka mingi sasa, naja nikitafuta matunda ya sifa na ibada kwa mtoto huyu,
lakini sipati kitu, mbona hata anawamalizia wenzake hewa? Hebu mkate
mara moja. Afya yote hii inakwenda bure tu! na nguvu zote hizi zinapotea bure
tu! Hebu wee malaika, chukua upanga, halafu Kata! (Waislam waamini huyo
malaika anaitwa Israeli)
Bwana Yesu, ndiye anayedumu
kutuombea.
Unajua, pamoja na hasira zote za Mungu Baba,
Biblia inasema, Yesu Kristo ndiye anayedumu kutuombea? (Warumi 8:34). Kwahiyo,
Bwana Yesu alipomsika Baba akiongea habari za kutaka kukuondolea mbali duniani,
kwasababu haumzalii Mungu matunda ya sifa na ibada aliyotamani sana kwako, mimi
binafsi naweza kumwona Bwana Yesu katika mawazo yangu tu, kwa ghafla, akiacha
kila kitu alichokuwa anafanya, halafu anamgukia Mungu Baba, akijua Mzee
hatanii. Ndipo Bwana Yesu anaamua kuingia katika maombezi, kwa ajili yako
(1Timotheo 2:5, Warumi 8:34)
Ndipo Yesu anakuja kwa Baba, kama mwombezi wetu na
kusema;
‘Baba, najua mtoto huyu
hajakuzalia matunda ya sifa na ibada kama tulivyotamani, lakini Baba, mbona kwa
mtoto huyu, ni daktari mzuri, anatibu watu vizuri au mbona mtoto ni mkulima
mzuri, analisha watu wote hawa? Hatuwezi kumuacha tu kwa hilo? Nakusihi
tusimkate mtu huu’. Lakini
naweza kumwona Baba mawazoni kwangu akisema, No! Sitaki, hicho kipawa chake
cha udaktari au ukulima, ni secondary (yaani ni kitu cha pili) lakini kitu cha
kwanza, yaani primary, mimi hapa nilikuwa nataka matunda! Matunda ya kusifiwa
na kuabudiwa! Nukta! Nimesema mwondoe!!
Pengine Bwana Yesu mwombezi wetu, (kama vile yule
mtunza shamba) anarudi tena kwa Mungu Baba, akiwa pamoja na Roho Mtakatifu,
wanatuombea tena na kumsihi Baba tena na kusema;
‘Baba wa rehema, najua mtoto huyu
hakuzalii matunda ya sifa na ibada kama tunavyotamani, lakini kumbuka kwamba,
kupitia kwa mtoto huyu huyu, ndipo tunapopata makochi mazuri na ndiye
anayetengeneza magari yote na mitambo yote ya viwanda vya mji huu! Mzee, nakusihi
tusimkate mtu huyu’.
Lakini Mungu Baba akasema hivi,
‘Nimesema No! Hivi wee Yesu na Wee
Roho Mtakatifu, Nimesema hiviiiii, Huyu mtu huti, amenichosha, sitaki kumuona
katika shambani langu, Nimekataa! Nasema hiviii, mkata huyu mtu! Mwondoee!
Hivyo vipawa vyake na taaluma zake unazosema zinawasaidia wenzake duniani,
kwangu mimi hizo, ni namba mbili na tatu; Lakini kitu cha kwanza kabisa,
nilichokuwa nakitaka kwa mtoto huyu, (yaani cha primary kabisa), mimi nilikuwa
nataka matunda! Matunda ya sifa na ibada kutoka kwake. Nukta! Lakini kwasababu
ameshindwa kutambua hilooooo, nimesema hiviiii, kata kabisa mtu huyu duniani,
Mwondolee mbali kabisa!!!
Duuh! Pengine Bwana
Yesu pamoja na Roho Mtakatifu, kwa mara ya mwisho kabisa kwarudi kwa Baba na
kumsihi, na tena safari hii, Bwana Yesu na Roho Mtakatifu mwombezi wetu,
wakamrudia Baba, kwa maombi mazito ya kuugua vile mtu asivyoweza
kutamka, (Warumi 8:26) na hata kuanguka na kumpigia Baba magoti kabisa
na wakamsihi wakisema;
‘Baba wa rehema, tunakuomba sana,
tunaugua kwa niaba ya huyu mtoto, Mimi na Roho Mtakatifu, tupo tayari kwenda
duniani, tukaishi na watoto wote hawa wanokuudhi na kukukasirisha kwa mwenendo
wao; Baba, mimi niko tayari kuchukua dhambi zake, hata kufa kwa ajili yake ili
tu nimwokoe na adhabu yako; Baba, nakusihi, hebu usimkate mtu huyu, nakuomba
sana, hebu mwache kwa mwaka huu mmoja nao, ili nimpelekee wahubiri na waalimu
wa neno la Mungu, tuone kama ataanza kukuheshimu.
Baba, hebu niache nimpelekee
na kitabu cha somo la kusifu na kuabudu, nimfundishe kwa upya, nimpalilie, tena
niutilie na samadi zaidi kidogo, na kuumwagilia maji zaidi kidogo, ili tuona
kama atabadilika tabia na ataanza kuzaa matunda ya sifa na ibada. Baba, kama
mtu huyu hapo baadaye, atakuzalia mtunda unayotaka, basi ni vema; lakini laa,
kama usipozaa, bali akaamua kupuuza mafundisho haya na kutobadili tabia yake
hii, basi nakuruhusu, unipe mimi mwenyewe upanga mkali, name nitakwenda
mwenyewe, kumkatilia mbali na shamba lako Mzee.
Basi kwa sababu hiyo tu, ndiyo maana Mungu ameghairi hasira zake zote
alizokuwa nazo juu yako, hata leo ungali unaishi ili tu uweze kufikishiwa
mafundisho haya mkononi mwako, na amekuongezea muda fulani wa kuishi, ili
pengine utabadilika na kuanza kumhasimu Mungu, na kumzalia matunda ya sifa na
ibada kwa Mungu, ambayo amekuwa akitamani sana kuyapata.
Mtu wa Mungu, ni muhimu sana
utambue kwamba, jambo la kwanza kwa uthamani na umuhimu mbele za Mungu, ni
sisi wanadamu tuwe vyombo vizuri vya sifa na ibada kwa Mungu. Hili
ndilo la kwanza kabisa, katika maisha yako, yaani primary! Yaani la kwanza
kabisa kuliko yote. Yaani ni muhimu ujue
kabisa ya kwamba, tumepewa uwezo na Mungu, uwezo wa kupumua na kutembea na
kufanya kazi, ili tuweze kutengeneza mazingira mazuri ya kimaisha, ili hatimaye
tuwe vyombo vizuri vya kumsifu Mungu na kumwabudu.
Mungu anathamini sana sifa na ibada.
Mpendwa, kama tulivyoona hapo juu, Mungu wetu
anathamini sana na anapenda sana kusifiwa na sisi watoto wake. Na ndio maana anataka
kusifiwa. Tumesoma kwamba, na ndiyo maana kule mbinguni, amejizungushia malaika
elfu elfu nyingi, wanaomsifu na kumwabudu yeye, kila siku, tena kwa masaa 24
mfululizo, mchana na usiku, bila kupumzika. Ni maelfu na maelfu ya malaika
wengi, wamekizunguka kiti chake cha enzi. Hiyo itakusaidia kuelewa jinsi Mungu
wetu alivyo very serious kuhusu sifa na ibada.
Tumesoma, wale malaika wanamwambia Mungu kwamba, Vitu vyote vimeumbwa na Mungu ili kutimiza mapenzi ya Mungu (Tafsiri zingine
zinasema mahitaji ya Mungu au matakwa ya Mungu). Kwahiyo, mapenzi
ya Mungu ya kwanza ni kusifiwa. Au mahitaji ya Mungu ni kusifiwa au matakwa
ya Mungu ya kwanza ni kisifiwa na kuabudiwa. Hivyo basi, sisi sote na viumbe
wote, tumeumbwa na Mungu duniani, ili tuwe kwake kama vyombo maalum vya kumsifu na
kumwabudu yeye Mungu. Kusifu
na kuabudu kunatupa sababu na maana ya sisi viumbe kuishi. Na ndio maana Daudi alipoelewa ufunuo huu.
Mfalme Daudi alipofunuliwa kusudi la Mungu juu ya
maisha yake, akajiambia mwenyewe, akasema “… Ee nafsi yangu, umsifu Bwana”. Halafu
katika mstari wa 2, anatuambia sisi wengine kwamba
“Nitamsifu
Bwana, muda ninaoishi, nitamwimbia Mungu wangu
ningali ni hai” (Zaburi 146: 1-2).”
Na Roho Mtakatifu alipompa Mfalme Daudi ufunuo
huu; Kwamba viumbe wote ni vyombo maalum vilivyoumbwa kumsifu na kumwabudu
Mungu, Daudi akaandika wimbo mwingine, katika kitabu cha Zaburi 150. Daudi anasema, au anatuamuru watu wote, tumsifu Bwana
kwa mazeze, filimbi, vinubi, tarumbeta, panda na matoazi mbalimbali yote,
yaliayo sana, na katika sehemu ya mwisho ya hiyo Zaburi hii, Mtumishi wa Mungu
Daudi anasema; “Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana” (Zab 150:6). Katika mstari
huu muhimu sana, tunaona Mfalme Daudi akisema, kila mwenye pumzi na amsifu Bwana.
Angalia vizuri, Daudi hakusema, Kila
mwenye sauti nzuri, amsifu Bwana. No! Wala hakusema, Kila mwenye kujua kupiga kinanda au gitaa,
ndiye anayestahili kumsifu Bwana. Bali alisema, kila mwenye pumzi, na amsifu
Bwana (Zab 150:6). Haya ni maneno mazito sana.
Kwa lugha nyingine, Daudi anamaanisha kwamba, kama
unakuwa bize (busy) sana kiasi cha kutokupatikana ibadani, mbele za Mungu, basi
kumbe wewe, hauna stahili ya kuitumia pumzi ya Mungu, tunayopewa wote, tena
bure kabisa bla kulipia, kama vile tunavyolipia simu zetu kwa vocha. Daudi
anasema kwamba, mtu wa namna hiyo, hana sababu ya kuendelea kupewa pumzi na
Mungu.
Haya si maneno rahisi ndugu yangu. Tafakari!
Kwahiyo, katika sehemu hii ya kwanza, nimetamani
ujue mambo haya muhimu, ili uweze kusimama na kutembea katika mapenzi ya Mungu.
Mungu anatamani sana kupata muda na wewe. Si kila wakati ukipata muda wa
kuomba, unatakiwa upeleke mahitaji yako na matatizo yako tu. Sikiliza, Mungu
anajua tunahitaji nini, kabla hata hatujamwomba. Bali Mungu anachotaka, ni sisi
watoto wake, tujifunze kutenga muda, wa kumsifu na kumwabudu yeye, kwa uzuri
wake, kwa uweza wake, kwa matendo yake makuu aliyotenda na aliyotutendea, na
tumsifu pia kwa ahadi zake. Na hapo, Biblia inasema kwamba, tukijifurahisha kwa
Bwana Mungu wetu, yeye atatupa zile haja za mioyo yetu, tulizonazo (Zab 37:4).
Mungu pia anataka kupendwa na kusifiwa (Kumb 6:4-9).
Na ndio maana Mfalme Daudi alikuwa rafiki wa
karibu sana na Mungu, ni kwasababu Daudi alijua kitu ambacho Mungu anakitaka
zaidi au anakipenda zaidi. Pamoja na kwamba, Daudi alikuwa na mahitaji mengi tu
kama sisi tulivyo nayo, lakini Daudi alijua namna ya kuuteka moyo wa Mungu;
Daudi alijua kwenda mbele za Mungu, kumsifu, kumshukuru na kumwabudu tu, pamoja
na kwamba ana mambo kibao yamemfika mpaka shingoni na kumkaba koo lake.
Sikiliza haya maneno ya Daudi, anasema hivi; Pamoja na kwamba nina matatizo
pia, tena mengi tu, lakini pamoja na hayo, mimi…
Jambo moja ndilo nimelitaka
kwa Bwana, nalo ndilo nitakalolitafuta, nikae nyumbani mwa Bwana, siku zote za
maisha yangu, niutazame uzuri wa Bwana, na kutafakari hekaluni mwake. (Zaburi
27:4)
Kwahiyo, pamoja na kwamba, Daudi alikuwa na
mahitaji mengi tu kama sisi tulivyo nayo, lakini huyu mpendwa alijua namna ya
kuuteka moyo wa Mungu; alijua namna ya kwenda mbele za Mungu, kumsifu,
kumshukuru na kumwabudu kwa moyo wake wote, utafikiri hana matatizo kabisa. Na
Mungu akapendezwa na moyo huo, akampa haja zote za moyo wake, hata zile ambazo
alikuwa bado anaziwaza tu, kabla ya kuziomba, Mungu akampa zote pia. Soma Zab
37:4 na Efe 3:20.