Wednesday, 3 July 2013

IJUE DHAMBI ISIYOSAMEHEKA. SEHEMU YA KWANZA.



HAIWEZEKANI KURUDI NYUMA

Mambo ya Kweli Yanayoshangaza

Maneno ya mkataa [ya kuamua mwisho wa mambo] yaliyopata kunenwa na Yesu yalihusu uwezekano wa kutisha wa kutenda DHAMBI ISIYOSAMEHEKA. Alisema, “Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa KUMKUFURU ROHO HAWATASAMEHEWA.” 12:3Mathayo 1. Hakuna mtu ye yote anayeweza kuuelewa vibaya ujumbe wa mafungu hayo. Kuna dhambi iliyo ya mauti. Mwanaume au mwanamke ANAWEZA KUVUKA MSTARI UNAOTENGANISHA REHEMA NA GHADHABU YA MUNGU, WALA ASIWEZE KURUDI NYUMA TENA. Maneno haya ya Bwana wetu yanayoushusha moyo na kuufanya uwe baridi yanasimama kinyume kabisa na maneno yake ya kawaida ya fadhili zake. Kwa sababu hiyo, kama hakuna nyingine, basi, ni lazima yachunguzwe kwa uangalifu mkubwa.
Ni dhambi gani hiyo ambayo Mbingu inaiangalia kwa karaha na machukio makuu? Kwa nini Mungu atawashughulikia kwa ukali mno wale walio na hatia ya dhambi hiyo? Kwa akili za kibinadamu matendo mengi sana ya upotovu na ukatili yanaweza kuangukia katika kundi hili, lakini ni tendo lipi miongoni mwa hayo ambalo Mungu angelihesabu kuwa ni baya na la kuogofya mno hata lisiweze kusamehewa? Mara chache, mtu hukutana na mtu anayeshangaa endapo ametenda dhambi hiyo. Sala zake zinaonekana kana kwamba zinarudia darini, naye haoni kwamba analo tumaini lo lote la kupata upendeleo au msamaha wa Mungu. Hata hivyo, yeye hawezi kuonyesha tendo moja lo lote la dhambi alilotenda ambalo limemtenga mbali na tumaini lake la wokovu. Anawezaje kujua kama ametenda kabisa ile dhambi isiyosameheka” Je, mtu anaweza kujua kweli?
Kabla ya kuyajibu maswali yote hayo yanayoleta kero [usumbufu] ambayo watu wanayauliza kuhusu dhambi hiyo isiyosameheka, pana haja ya kuijua kweli moja tukufu. Sisi tunamtumikia Mungu mwenye upendo na huruma isiyo na kifani. Si mapenzi yake kwamba mtu ye yote apotee [2 Pet. 3:9; 1 Tim. 2:4; Yn. 3:16]. Katika Neno lake yeye amefanya mpango kwa kila mtu kusafishwa na kutakaswa [Efe. 1:3-7; 1 Kor. 6:9-11]. Ahadi ya 1 Yohana 1:9 ambayo ni vigumu sana kuisadiki inamhusu kila mwanaume, mwanamke, au mtoto katika ulimwengu huu wa leo: “TUKIZIUNGAMA dhambi zetu, YEYE NI MWAMINIFU na wa haki hata ATUONDOLEE dhambi zetu, na KUTUSAFISHA na udhalimu wote.”
Kwa sharti hilo la UNGAMO LA KWELI, Mungu anaahidi kuisamehe dhambi ya aina yo yote, bila kujali ilivyo. “Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.” Isaya 1:18.
Ni ahadi ya pekee ilioje hiyo kwa wale walioivunja kila sheria ya Mungu na ya wanadamu, kwa kujitosa [kujitupa] kwao katika upotovu kama wenda wazimu. Mungu bado angali anawapenda! Hakuna dhambi iliyo kubwa mno kwake kuweza kushindwa kuiosha. Anangoja, mikono yake ikiwa imenyoshwa, kumpokea mtu ye yote anayechukua hatua ya kuelekea kwenye msamaha na rehema yake.
Picha kama hiyo ya Mungu inaonekana kuwa ni ngeni kabisa ukiilinganisha na maneno ya Yesu katika Mathayo 12:31,32. Ikiwa Baba yuko tayari sana kusamehe na kuokoa, kwa nini, basi, kuwe na kitu kama hicho cha dhambi isiyosameheka? Jibu lake ni rahisi. DHAMBI HIYO HAISAMEHEKI KAMWE KWA SABABU HAIUNGAMWI KAMWE. Haitubiwi kamwe. Mungu hatawalazimisha wenye dhambi kupokea msamaha wake. Ni lazima WATUBU wenyewe na KUUNGAMA. Hata ile ahadi nzuri sana ya 1 Yohana 1:9 ina neno lile la maana sana lisemalo “KAMA” [ -KI-] - “[Kama] tuKIziungama dhambi zetu….” Kwa mamlaka ya Neno hilo la Mungu, twaweza kuhakikishiwa ya kwamba kila dhambi itasamehewa KAMA tukiiungama kwa imani na kwa toba.
Mawazo mbalimbali yametolewa kuelezea kwa nini dhambi hiyo moja haiungamwi kamwe. Wengine wanaamini kwamba dhambi hiyo ni ya mtu kujiua mwenyewe; wengine wanadhani huenda ikawa ni uzinzi fulani wa kuogofya mno au kumtukana Roho Mtakatifu.
Jambo moja ni dhahiri - hiyo ni dhambi! Huo ndio mwanzo mzuri, kwa sababu Biblia inatoa tafsiri rahisi ya neno hilo baya sana la “dhambi.” “Kila mtu atendaye dhambi ANAVUNJA SHERIA YA MUNGU [Amri Kumi], MAANA DHAMBI NI UVUNJAJI WA SHERIA [Amri Kumi].” 1 Yohana 3:4, AJKK. Paulo anaupanua usemi huo kwa kutangaza kwamba dhambi ni uvunjaji wa Sheria ile ya Amri Kumi. “Walakini SINGALITAMBUA DHAMBI ILA KWA SHERIA [Amri Kumi]; kwa kuwa singalijua KUTAMANI, kama torati [Sheria/Amri Kumi] isingalisema USITAMANI [Kut. 20:17].” Warumi 7:7. Sio tu kwamba dhambi hiyo isiyosameheka inahusiana na kuivunja hiyo Sheria Kuu ya Maadili ya Mungu [Amri Kumi], bali pia ni kosa dhidi ya Roho Mtakatifu. Hali ya kosa hilo imefungamana kwa karibu sana na KAZI KUU ZA ROHO huyo. Yesu alisema, “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, ATAWAFUNDISHA YOTE, na KUWAKUMBUSHA YOTE niliyowaambia.” Yohana 14:26.
Mbali na kutufundisha sisi mambo yote, Yesu alidokeza kwamba huyo Roho pia angeweza kutu“ONGOZA a[tu]tie kwenye KWELI YOTE.” Yohana 16:13. [Kweli hiyo ni Neno na Amri Kumi – Yn. 17:17; Zab. 119:142.] Kila mwanafunzi anayelichunguza kwa makini Neno huenda ameonja mafundisho hayo, yaani, mvuto huo uongozao wa Roho Mtakatifu. Hapawezi kuwapo na ufahamu wa ndani wa kweli ya Biblia bila kutiwa nuru na Roho huyo wa Mungu. Utume wa [kazi ya] tatu wa Roho Mtakatifu ni KUTUHAKIKISHIA DHAMBI. Yesu alisema: “Yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo ATAUHAKIKISHA [ATAUTHIBITISHIA] ulimwengu kwa habari ya DHAMBI [uvunjaji wa Amri Kumi], na HAKI, na HUKUMU.” Yohana 16:7,8.
Ni kazi ya pekee ya huyo Roho kutukemea au kutuhakikishia dhambi zetu. Mabaya yanapotendwa, DHAMIRI INACHOMWA kwa hisia ya hatia. Tafadhali zingatia kwamba kadiri tunavyomruhusu Roho Mtakatifu KUTUFUNDISHA, KUTUONGOZA na KUTUHAKIKISHIA DHAMBI ZETU, hatuwezi kamwe kuwa na hatia ya kutenda dhambi hiyo isiyosameheka. Lakini hebu na tuseme kwamba sisi tunakataa katakata kuzitambua kazi hizo tatu za Roho Mtakatifu katika maisha yetu kuhusiana na Mungu, je, mambo yatakuwaje? Hapo ndipo mahali ambapo watu wanaikaribia mipaka ile ya kufisha ya kutenda dhambi hiyo mbaya kuliko zote zilizoandikwa katika kumbukumbu hizi.
Ni jambo la kuvutia sana kuchunguza kuenea kila mahali kwa dhambi hiyo katika kumbukumbu za Biblia. Wakati fulani mmoja uliopita karibu kila mtu katika dunia hii alikuwa amevuka mahali pale ambapo haiwezekani kurudi nyuma. “BWANA akasema, Roho yangu [Roho wangu Mtakatifu] haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini. Mwanzo 6:3. Mungu hapo anazizungumzia habari za watu wale walioishi kabla ya ile Gharika ambao waliangamia katika gharika ile. Kwa zaidi ya miaka mia moja Roho Mtakatifu [Roho wa
Kristo/Mungu – Rum. 8:9; 1 Pet. 3:18-20] alikisihi sana kizazi kile kiovu kwa njia ya mahubiri ya Nuhu [Kristo alihubiri kwa njia ya Roho wake kupitia kwa Nuhu]. Japokuwa mawazo ya moyoni mwao sikuzote yalikuwa ni mabaya tu, palikuwa na wachache, yaani, watu wale nane waliosalia ambao waliitikia wito wa yule Roho na kuingia katika safina ile. Wengine wote waliobaki walifagiliwa mbali na maji yale yaliyokuwa yamechafuka vibaya sana ambayo yalikuwa yameifunika kabisa kila inchi ya uso wa dunia hii. Baada ya miaka mingi ya kujitahidi kwa uvumilivu mkubwa , Roho akaondoka kabisa kwao na kuwaacha wapingaji wale shupavu ili wapate kukabiliwa na ajali waliyoichagua wenyewe.
Je, jambo hilo linaweza kutokea tena? Kuna mlandano wa kushangaza mno kati ya siku zile za Nuhu na siku zetu hizi. Yesu alisema, “Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu [Kristo].” Luka 17:26. Kufanya mambo kupita kiasi kule kule kunatendeka hivi sasa katika miji yote mikuu ya ulimwengu. Upotovu uliokithiri mno bado unazionyesha waziwazi tamaa mbaya za mwili zinazofuatiwa na kila taifa chini ya jua.
Kwa nini watu wale wengi sana walioishi kabla ya gharika walikataa kuingia katika safina ile ya usalama? Wengi wao walimsaidia kabisa Nuhu kuitengeneza meli ile kubwa sana. Roho Mtakatifu aliwachoma mioyo yao sana kwa kuwahakikishia dhambi zao, lakini hawakutaka kuachana nazo na kuutii ujumbe ule. Mwishowe Mungu akasema, “WAACHENI. Roho wangu hatashindana nao tena.”
Je, hivi kutakuwako na gharika nyingine [itakayoifunika dunia yote]? Ni kweli kabisa. Lakini itakuwa ni GHARIKA YA MOTO, ambayo itaiteketeza kabisa sayari hii pamoja na vyote vilivyomo ndani yake [2 Pet. 3:1-7,10]. Je, ni kwa jinsi gani ulimwengu huu unaitikia wito wa kuingia katika safina inayowalinda na kuwaweka salama? Roho yule yule anaendelea kuwasihi sana leo; ujumbe unaofanana na ule ambao unawatenga watu na kuwaletea uamsho unavuma kote [2 Kor. 6:14-18; Ufu. 18:4,5; 14:6-12]; na huyo Roho wa Mungu anaendelea kutendewa sawasawa na vile alivyotendewa katika siku zile za Nuhu.

KUMKUFURU ROHO MTAKATIFU
Nasoma mambo matatu katika Biblia ambayo watu wanayatenda dhidi ya Roho Mtakatifu. Kwanza kabisa, katika Waefeso 4:30: “Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.” Angalia kwamba watu wanaweza KUMHUZUNISHA ROHO MTAKATIFU, na Biblia inasema kwamba itakuwa hivyo katika siku hizi za mwisho.
Ni jambo gani tena watakalofanya dhidi ya huyo mwakilishi binafsi wa Mungu [Roho Mtakatifu]? Katika Waebrania 10:29 tunaambiwa kwamba watu WATAMDHARAU ROHO MTAKATIFU. “Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule anayemkanyaga Mwana wa Mungu [kuzivunja Amri Kumi ni sawa na kumkanyaga Kristo], na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na KUFANYIA JEURI ROHO WA NEEMA?” Neno hili “jeuri” lina maana sawa na “dharau.” Hebu basi fikiria hilo! Watamdharau Roho Mtakatifu. Basi na tuliweke jambo moja zaidi mbele yetu. Hilo limo katika Matendo 7:51: “Enyi wenye shingo gumu,
msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote MNAMPINGA ROHO MTAKATIFU; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vyvyo hivyo.” Basi hapa tunayo mambo matatu ambayo watu wanafanya ili kumkufuru Roho wa Mungu: WANAMHUZUNISHA, WANAMDHARAU, tena WANAMPINGA kama vile walivyompinga siku zile za Nuhu [Mwa. 6:3-8].
Je, ni athari gani zinazompata mtu kwa kufanya uasi wake wote huo dhidi ya Roho? Karibu kabisa bila ya yeye kutambua DHAMIRI YAKE HUCHOMWA MOTO [HUUNGUZWA (Seared) – 1 Tim. 4:2, KJV], na MOYO WAKE UNAKUWA MGUMU. Kwa kweli, hii ndiyo maana hiyo inahesabiwa kuwa ni dhambi ya kutisha. Mara nyingine watu husema, “Sijui kwa nini Mungu aweze kuifikiria dhambi hiyo kuwa ni kitu kibaya mno kiwezacho kufanywa.” Nitakuambia kwa nini: Kwa sababu ROHO MTAKATIFU NDIYE NJIA YA PEKEE AMBAYO KWAYO MUNGU ANAWEZA KUMFIKIA MWANADAMU [Yn. 16:7,8; Rum. 2:4,5; Mdo. 2:37-39; 7:54; Yak. 4:4-6].
Hakuna njia nyingine yo yote aliyo nayo Mungu ya kumwokoa mwanadamu isipokuwa kupitia kwa Roho wake Mtakatifu. Hiyo ndiyo njia ambayo kwayo tunaongozwa kwenye toba. Kama sisi hatunaye huyo Roho Mtakatifu, basi, hakuna tumaini lo lote [la uzima wa milele] linalobaki kwetu [Mdo. 5:30-33;
Rum. 8:9,11,14]. Ni kama mtu anayezama baharini akiwa peke yake, halafu mtu mmoja anakuja na kumtupia juya moja la kuokolea maisha yake. Kama mtu yule analishika juya hilo la kuokolea maisha, basi, anaweza kuokolewa, lakini kama akikataa kulishika juya hilo ambalo ni kiungo cha pekee na pwani kinachoweza kumpeleka ufukoni, basi, ataangamia bila tumaini lo lote. Vile vile, sisi tumo duniani humu, na njia ya pekee ambayo kwayo Mungu anaweza kutufikia sisi ni kupitia kwa Roho Mtakatifu.
Kama sisi tunampa kisogo Roho wake na kukataa KUMSIKILIZA NA KUMTII, basi, Mungu atatuacha, nasi tutapotea [Mwa. 6:3,5,7; Hosea 11:8,9; lakini hatimaye Hosea 4:17]. Hii ndiyo maana Daudi alikuwa na wasiwasi sana katika sala yake kuu ya toba. Alipokuwa akifichua yote yaliyo moyoni mwake kwa Mungu katika Zaburi ya 51, Daudi alisema, “Usinitenge na uso wako, wala ROHO [W]AKO MTAKATIFU USINIONDOLEE.” Fungu la 11. Alitambua ya kwamba endapo Mungu angemwondoa kwake huyo Roho Mtakatifu, basi, yeye angekuwa amepotea kabisa. Angeachwa peke yake bila kuwa na njia nyingine yo yote ya kuokolewa. Na hii ndiyo maana Yesu alisema kwamba hiyo ndiyo dhambi isiyosameheka [kwa kuwa mtu hawezi kabisa kutubu bila Roho – Ufu. 16:9,11,21]. Wewe unapojitenga mbali na kukataa kumsikiliza Roho Mtakatifu, basi, hakuna tumaini lo lote kwako.

NJIA TATU ZA KUFANYA DHAMBI DHIDI YA ROHO
Hapa nimeziorodhesha njia tatu ambazo kwazo watu wanaweza kuitenda dhambi hii [ya kumkufuru Roho]. NJIA YA KWANZA, ni mtu kusema hivi tu, “SITAKI KUOKOLEWA; sitaki mtu ye yote anisumbue juu ya Mungu, wala Biblia.” Si mara nyingi utakutana na mtu kama huyo. Nafurahi kukuambia kwamba si mara nyingi. Watu wengi sana kwa kweli wanataka kuokolewa [sio kulokoka], lakini mara kwa mara utawakuta wengine ambao hawana hamu kabisa ya kuokolewa. Wameridhika kabisa na mambo ya ulimwengu huu yanayokidhi tamaa zao mbaya za mwili. Hebu zingatia isemwavyo katika Mithali 28:13. “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; bali yeye AZIUNGAMAYE NA KUZIACHA atapata rehema.” Wale wasiotaka kuachana na dhambi zao hatimaye watajituliza wenyewe na kusema kwamba wanayo furaha bila kuwa na Kristo. Hatimaye hawatasikia kushtakiwa ko kote na dhamiri zao, na Roho Mtakatifu ATAWAACHA peke yao.
Kundi la pili ambalo linaathiriwa vibaya sana na dhambi hiyo linaifikia kwa kupitia NJIA NYINGINE [YA PILI]. Wao wanataka kuokolewa kweli kweli, nao wanamwambia kila mtu kwamba ni jambo walilolipa kipaumbele kwa ajili ya maisha yao ya baadaye kuishi kwa amani na Mungu. Kwa bahati mbaya, kundi hili linazidi KUNGOJEA UTAKAPOKUJA WAKATI MZURI UNAOFAA KUJITOA KABISA KWA MUNGU. Wao wakiwa na nia njema yote hiyo, wanaziacha nafasi nzuri za thamani kupita mpaka hapo nia zao zinapopooza kwa kukosa kwao uwezo wa kuamua la kufanya. Watu kama hao bado wanaendelea kuongea juu ya kumfuata Kristo njia yote, lakini uwezo wao wa kutenda umeharibiwa kwa KUSITA-SITA KWAO. Mwishowe watakuwa wamechelewa-chelewa mno na kupavuka mahali pale ambapo kwao haiwezekani kurudi nyuma.
Bila shaka kundi kubwa sana la wenye dhambi isiyosameheka linapatikana katika kundi la tatu [NJIA YA TATU] ambalo nataka kuzungumza habari zao. Ni ajabu ya kutosha, watu hao wanaonekana kuwa karibu hawana mwelekeo kabisa wa kuitenda dhambi hiyo isiyosameheka. Wao ni washiriki wa kanisa - huenda hata wamekuwa nguzo katika usharika wao. Je, hilo linakushtua sana? Kwa nini Wakristo hao wawe katika hali ya hatari sana ya kutenda dhambi hiyo kuliko makundi yale mengine mawili? Kwa sababu WAO HAWAJUI KWAMBA KWELI INAZIDI KUFUNULIWA ZAIDI NA ZAIDI [Mithali 4:18]. Mamilioni ya Wakristo wamekaa raha mustarehe katika viti vyao vyenye raha makanisani mwao wakijikinai [wakijisifu mno] kwamba wao WAMEOKOKA. Wanajiona kwamba wao wako salama kabisa wanapoendelea kuzifuata desturi za kanisa lao, wasitambue kwamba ubatizo ni mwanzo tu wa safari yao ndefu ya KUKUA katika maisha yao ya Kikristo [2 Petro 3:18; Efe. 5:17; Mdo. 17:26,27,30,31].
Alisema hivi Mtunga Zaburi: “NENO lako ni TAA ya miguu yangu, na MWANGA wa njia yangu.” Zaburi 119:105. Kadiri tunavyokwenda na kuingia ndani zaidi katika Biblia, ndivyo kadiri zinavyozidi kufunuliwa kweli nyingi zaidi, na ndivyo uwajibikaji wetu mbele za Mungu unavyozidi kuongezeka. Hajamfunulia kweli yake yote mtu mmoja awaye yote kwa wakati mmoja [Yn. 16:12-15; 14:26; Mt. 28:19,20]. Taa hiyo inaangaza mbali kiasi cha kutosha kumwezesha mtu ye yote kwenda mbele hatua moja kwa salama. Tunapopiga hatua ile, HATUA NYINGINE INAONEKANA MBELE
YETU. Tunapokua katika neema na maarifa, Mungu anataka sisi tuendelee kusonga mbele kuifuata nuru ya ile kweli inayoangaza mbele yetu.

DHAMIRI INAUNGUZWA KWA KUTOTII KWETU
Basi na tuseme kwamba mimi naiona nuru kutoka katika taa ya Neno la Mungu, lakini NAKATAA KUITII. Hebu na tuseme kwamba Roho Mtakatifu amenichoma moyo wangu na kunionyesha dhambi yangu [Yn. 16:8; Mdo. 2:37,38], nami najua vizuri kabisa anachotaka kwangu, lakini mimi sipendi kabisa, tena naona haifai kuachana na kitu hicho. Hivi kutatokea nini kwangu mimi ninapoendelea kuipuuzia nuru hiyo na kuikataa kweli aliyonifunulia Roho - kwa msingi wa sababu yo yote ile niliyo nayo? Naam, Roho ataendelea kusema nami, na kwa muda fulani nitaona vita ndani ya dhamiri yangu.
Nitajisikia mnyonge na mwenye hatia. Siku zitapita, na hata miezi itapita, wakati mimi naendelea kufanya kinyume na vile dhamiri yangu inavyonionyesha lile lililo jema kwangu kulitenda. Taratibu, DHAMIRI YANGU ITAANZA KUJIREKEBISHA NA KUAFIKIANA NA KILE KINACHOFANYIKA MWILINI MWANGU. Polepole hisia zangu za dhambi zitaanza kupungua, na matendo yale ya uasi [kutotii] kidogo kidogo yataanza kuonekana kuwa si ya kuchukiza sana.
Hatimaye, ile kweli iliyoonekana kwamba inaeleweka wazi kabisa kwetu, wala haikuwa na utata wo wote pale mwanzo, itageuka na kuwa dimbwi la matope la MASHAKA. Sababu mbalimbali zitajitokeza za kuhalalisha uasi huo, na zile hisia za dhambi tulizokuwa nazo mwanzoni zitaendelea kufifia. Maisha yatakuwa ni ya raha karibu sawa na vile yalivyokuwa kabla nuru hiyo haijaja kwetu. Ni jambo gani litakuwa limetokea? Tutakuwa tumetenda dhambi dhidi ya Roho Mtakatifu, nasi tutaanza kuzama na kuingia katika hali ya kuitenda ile dhambi isiyosameheka. Unajua, DHAMBI HIYO YA KUFISHA SI TENDO LO LOTE LILILO DHAHIRI AMBALO LINAWEZA KUTENGANISHWA NA KUTAJWA KWA JINA LAKE. INAWEZA KUWA NI DHAMBI YO YOTE INAYOTUNZWA MOYONI baada ya kuipokea hiyo nuru na maarifa. Hasa hasa ni HALI INAYOTOKANA NA KUFA GANZI KWA DHAMIRI inayosababishwa na uasi wa kudumu dhidi ya ile kweli tunayoijua [Efe. 4:17-19]. Matokeo yake ni sawa na kuipuuzia kengele ya saa. Dhamiri inageuka na kuwa katika hali ya kustahimili kuchomwa-chomwa moyo kunakokumbusha uasi huo mpaka mwishowe, HAITAWEZA KUTAMBUA [KUSIKIA] TENA KUCHOMWA-CHOMWA MOYO HUKO isikokutaka kabisa ambako kunasababishwa na hatia ya dhambi ile iliyotendwa. Kama ilivyo saa, dhamiri nayo pia inapungua nguvu yake kwa kuwa hakuna anayesikiliza tena.
Je, umeanza kuona kwamba mambo yote kwa kweli hutegemea kile tunachofanya na ile kweli? Yakobo aliandika hivi, “Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala HAYATENDI, kwake huyo NI DHAMBI.” Yakobo 4:17. Ni mamoja kwetu endapo sisi ni matajiri au maskini, Wakatoliki au Wayahudi au Waprotestanti, hoja kuu inahusu kama sisi tunatenda kile tunachokijua [Yak. 2:22; Luka 6:46-49; 11:27,28; Mt. 7:21-27].
Yesu aliielezea kwa mapana zaidi kanuni hiyo ya maana sana. Alisema, “Kama nisingalikuja na kusema nao, WASINGALIKUWA NA DHAMBI; lakini sasa HAWANA UDHURU kwa dhambi yao.” Yohana 15:22. Ni nani, basi, anayewajibika na kushtakiwa mbele za Mungu? Ni wale waliotiwa nuru na Roho Mtakatifu kutoka katika Neno lake. Watu walio waaminifu kwa yale yote wanayoyajua, yawe mengi au machache, watakubaliwa [na Mungu]. Dhambi itahesabiwa tu dhidi ya wale WALIOISIKIA KWELI NA KUIKATAA KABISA [Luka 12:45-48].
Kristo alisema, “Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa.” Yohana 9:41. Tatizo lote hilo la dhambi hiyo isiyosameheka linazunguka katika HOJA YA UTII KWA KILE TUNACHOKIJUA. Safari nyingine Yesu alisema, “Enendeni maadamu mnayo nuru, giza lisije likawaweza.” Yohana 12:35. Hivi nuru hiyo inatoka wapi? Ni Roho Mtakatifu anayetutia katika kweli yote [Yn. 16:13; 17:17; Zab. 119:142]. Sisi tunapokataa katakata kuitii hiyo kweli, basi, tunaikataa huduma ya Roho ambaye peke yake ndiye anayetuunganisha sisi na wokovu.
Tunamfukuza kabisa huyo Mmoja ambaye Mungu amemtuma kutuokoa sisi. Je, waweza kuona sana jinsi jambo hili linavyoweza kumwangamiza mhusika? Mjumbe huyo wa pekee wa Mungu anahuzunishwa na kuondoka kwa kukataa kwetu kwa makusudi kuupokea mwaliko wake wa rehema. Hapo kale Mungu alisema, “Roho wangu
hatashindana na mwanadamu milele [Mwa. 6:3, KJV]. Hatimaye Mungu atamwambia Roho wake Mtakatifu, atasema, “WAACHENI. Kama wanang’ang’ania kuifuata njia yao wenyewe, usiwatafute tena.” [1 The. 5:19; Mithali 16:25.]

DINI YA WAZAZI WETU HUENDA ISIWE NZURI KIASI CHA KUTOSHA
Labda maelezo yaliyo sahihi kabisa ya dhambi isiyosameheka katika Agano Jipya ni yale
yanayopatikana katika Matendo 7:51: “Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, SIKU ZOTE MNAMPINGA ROHO MTAKATIFU; kama BABA ZENU walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.” Watu hao walipiganaje na Roho wa Mungu? Stefano anasema kwamba walifanya hivyo kwa KUJIFICHA NYUMA YA DINI YA BABA ZAO. Wao WALIFUATA NJIA YA DINI ILE ILE TU WALIYOPITA WAZAZI WAO. Je, kuna ubaya wo wote kwa jambo hilo? Katika mfano huo tuliopewa palikuwa na ubaya, kwa sababu fungu hilo linaendelea kuwaeleza kama ni wale wa“lioipokea torati (Sheria ya Mungu ya Amri Kumi) kwa agizo la malaika, [wa]siishike.” Fungu la
Je, unaiona picha hiyo? Bila kujali wazazi wao walivyoelewa, watu hao waliipokea Sheria [Amri Kumi] ambayo Mungu aliwataka kuitii. Kila kizazi na kila mtu atahukumiwa kwa msingi wa KILE ANACHOKIJUA na jinsi ANAVYOKITII. Hakuna dini ya mtu ye yote iliyo nzuri kiasi cha kutosha kwa mtu mwingine kwa sababu kuna viwango vinavyohitilafiana vya uwajibikaji kwa kila mtu. Babu yangu angeweza kuokolewa kwa kufuata nuru aliyokuwa nayo, lakini mimi nisingeweza kuokolewa kwa kufanya jambo lile lile alilolifanya yeye. Mimi nina kipimo tofauti cha ile kweli iliyokwisha kufunuliwa kwangu ambayo kwayo Mungu atanishikilia mimi kuwa ninawajibika.
Ukweli ni kwamba mtu ye yote anamkataa na kumdharau Roho Mtakatifu wakati ule anapoivunja kwa makusudi amri yo yote ya Mungu. Kwa mujibu wa Biblia, Roho hawezi kukaa katika maisha ya mtu ye yote asiyetii. “Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na ROHO MTAKATIFU AMBAYE MUNGU AMEWAPA WOTE WAMTIIO.” Matendo 5:32. Tena, Yesu alisema: “Mkinipenda mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili Baba, naye atawapa Msaididi Mwingine, ili akae nanyi milele.” Yohana 14:15,16.