KUMCHA MUNGU
KUNA FAIDA
Ndugu wapendwa katika bwana
nawasalimu katika Jina la BWANA WETU YESU KRISTO
Leo katika mfululizo wetu wa
kuwaletea neon la uzima yaani chakula cha kiroho tunawaletea neon lenye kichwa
hicho hapo juu. Endelea kufuatana na
sisi kila wakati upate kuimarisha imani yako.
Malaki 3: 13-18
Maneno
yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema BWANA. Lakini ninyi mwasema, Tumesema
maneno magumu juu yako kwa namna gani? 14Mmesema; Kumtumikia Mungu hakuna
faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa
huzuni mbele za BWANA wa majeshi? 15Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio
walio heri; naam, watendao maovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio
waponywao. 16Ndipo walio mcha BWANA waliposemezana wao kwa wao. Naye BWANA
akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake,
kwa ajili ya hao aliomcha BWANA, na kulitafakari jina lake. 17Nao watakuwa
wangu, asema BWANA wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; watakuwa hazina
yangu hasa; naami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe
amtumikiaye. 18Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na
waovu, kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia”
Kuna
watu, na pengine nawe ni mmoja wao, ambaye baada ya kukaa katika maisha ya
kumtafuta Mungu na kuona hapati alichotarajia, hugeuka na kuanza kulalamika.
Hulalamika kwa kuona kama amejitaabisha bure katika kujiepusha na uovu wa dunia
hii. Huona kama amejizuwia kutenda maovu pasipo kuwa na faida. Anaweza hata
kushawishika anapowaona watu wakifurahia dhambi akajiona yeye anaishi maisha ya
huzuni pasipo na sababu [ingawa kumcha Bwana ni furaha kubwa].
Pengine
mtu amekuwa akifunga na kuomba ili jambo fulani litokee. Na kinyume chake
akawaona wale ambao hata jina la Yesu halijawahi kutamkwa vinywani mwao ndio
wanaofanikiwa. Ndio wanaojenga majumba makubwa, na wengine kuyaita kwa majina
yao; akaona wale wanaotoa rushwa maofisini ndio wanaoongezewa mishahara na
kupandishwa vyeo, huku yeye akiwa ameishikilia haki, yuko katika nafasi ile
ile.
Yawezekana
kuna mtu amekuwa anasumbuliwa na ugonjwa fulani kwa muda mrefu, ameomba sana
lakini ugonjwa huondoki. Halafu akiangalia upande wa pili anaona kuna mtu
ambaye alikwenda mara moja tu kwenye maombezi kisha akapona; na baada ya kupona
mtu huyo alirudi tena dhambini, yaani kupona kwake ndio kumempa nguvu zaidi ya
kutenda maovu. [3:15]Huyo aliyekuwa anamjaribu Mungu ndiye amepona halafu yeye
bado anaumwa!
Sikiliza
Neno la Mungu lisemavyo katika ule mstari wa 16 “Ndipo walio mcha BWANA
waliposemezana wao kwa wao. Naye BWANA akasikiliza, akasikia; na kitabu
cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao aliomcha BWANA, na
kulitafakari jina lake”
Jambo
muhimu kulifahamu hapa ni kitu walichosemezana wao kwa wao, hao wamchao
BWANA. Lakini bila shaka hao wamchao Bwana walisemezana juu ya ukuu wa Mungu!
Walifarijiana na kutiana moyo kuwa japo wanapita katika mapito bado BWANA Mungu
ndiye nguvu yao. Walifarijiana kwamba hata kama walichofunga na kukifanyia
maombi hakikutokea bado BWANA Mungu ni tumaini lao!
Ni
kama tu walivyosemezana akina Shadraki, Meshaki na Abednego kuwa hata kama
BWANA Mungu asipowaokoa katika lile tanuru la Moto lakini wao hawakuwa tayari
kuisujudia ile sanamu ambayo mfalme Nebukadreza aliyokuwa ameisimamisha!
[Daniel 3].
Wamchao
waliposemezana BWANA alisikiliza na akasikia wakiongea maneno
yenye kuelekeza kwake tumaini lao lote. Baada ya BWANA kusikia maneno hayo pale
pale kitabu cha ukumbusho kiliandikwa mbele zake wa ajili yao kwa kuwa
walisemezana maneno mema huku waliendelea kulitafakari jina lake!
Tusidanganyike! Kumtumikia BWANA Mungu kuna faida. Kuokoka
kuna faida. Waache wanaofanikiwa kwa njia za ufisadi wafanikiwe. Waache
wanaochekelea katika furaha ya dhambi, ambayo ni ya kitambo kidogo sana,
waendelee[Ebrania
11:25]. Waache wanaojiunga katika imani potofu kwa ahadi za utajiri
waendelee, maana siku itakapofika utajiri huo hautakuwa na msaada wowote kwao.
Waache wanaotafuta uponyaji kwa njia zisizo za ki-Mungu waendelee maana iko
siku ambayo itakuwa kama vile magonjwa hayo yamerudi yote kwa wakati mmoja!
Lakini
pia iko siku BWANA ataondoa tabu yako. Pengine ameacha shida, ugonjwa au adui
huyo aendelee kukusumbua kwa kusudi akufundishe jambo. Pengine ameacha ili
akujaribu moyo wako umeweka wapi msingi. Pengine ameacha ili akujaribu unataka
mema tu toka kwake au hata mabaya? [Ayubu 1:10]. Yawezekana ameacha ili akuone
kama uko tayari kufa kwa ugonjwa huku bado sifa zake zikitoka kinywani mwako na
wala hautamkufuru. Pengine amaecha hayo ili uendelee kunyenyekea. [2Kor 12:7].
Pengine ameacha hayo ili akutukuze, akufanye mfano wa Ayubu, ili uwe mfano wa
kuigwa katika vizazi na vizazi!
Hebu
tuendelee kumtumaini BWANA Mungu. Tuendelee kumuisha yeye. Tuendele kujitia
nguvu katika yeye. Tunapokutana tusemezane maneno ya Neema hii aliyotupatia,
Neema ya Wokovu. Tunapokuata tuliitie jina lake. Hapo ndipo tutaweka rekodi
mbinguni! Loh! Ni fahari iliyoje mcha Mungu kuongea huku duniani kisha mambo
hayo yakaandikwa mbinguni!
Kumcha
BWANA kuna faida! Tudumu katika hilo kwa kuwa katika siku ile tutakuja
kutambulika kama tulikuwa tunamcha BWANA Mungu, kama kweli tutadumu katika
kumcha Yeye! Na hapo ndipo kutakuwa na malipo kwa wenye haki, Uzima wa
milele na waovu, adhabu ya milele!
Mungu
atusaidie!
The Blogger Bishop to be Mgalula, Y.J.