HAIWEZEKANI KURUDI NYUMA
Mambo
ya Kweli Yanayoshangaza
Maneno
ya mkataa [ya kuamua mwisho wa mambo] yaliyopata kunenwa na Yesu yalihusu
uwezekano wa kutisha wa kutenda DHAMBI ISIYOSAMEHEKA. Alisema, “Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na
kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa KUMKUFURU ROHO
HAWATASAMEHEWA.” 12:3Mathayo 1. Hakuna mtu ye yote anayeweza kuuelewa vibaya ujumbe wa mafungu
hayo. Kuna dhambi iliyo ya mauti. Mwanaume au mwanamke ANAWEZA KUVUKA MSTARI
UNAOTENGANISHA REHEMA NA GHADHABU YA MUNGU, WALA ASIWEZE KURUDI NYUMA TENA.
Maneno haya ya Bwana wetu yanayoushusha moyo na kuufanya uwe baridi yanasimama
kinyume kabisa na maneno yake ya kawaida ya fadhili zake. Kwa sababu hiyo, kama
hakuna nyingine, basi, ni lazima yachunguzwe kwa uangalifu mkubwa.
Ni dhambi gani hiyo ambayo Mbingu inaiangalia kwa karaha na
machukio makuu? Kwa nini Mungu atawashughulikia kwa ukali mno wale walio na
hatia ya dhambi hiyo? Kwa akili za kibinadamu matendo mengi sana ya upotovu na
ukatili yanaweza kuangukia katika kundi hili, lakini ni tendo lipi miongoni mwa
hayo ambalo Mungu angelihesabu kuwa ni baya na la kuogofya mno hata lisiweze
kusamehewa? Mara chache, mtu hukutana na mtu anayeshangaa endapo ametenda
dhambi hiyo. Sala zake zinaonekana kana kwamba zinarudia darini, naye haoni
kwamba analo tumaini lo lote la kupata upendeleo au msamaha wa Mungu. Hata
hivyo, yeye hawezi kuonyesha tendo moja lo lote la dhambi alilotenda ambalo
limemtenga mbali na tumaini lake la wokovu. Anawezaje kujua kama ametenda
kabisa ile dhambi isiyosameheka” Je, mtu anaweza kujua kweli?
Kabla ya kuyajibu maswali yote hayo yanayoleta kero
[usumbufu] ambayo watu wanayauliza kuhusu dhambi hiyo isiyosameheka, pana haja
ya kuijua kweli moja tukufu. Sisi tunamtumikia Mungu mwenye upendo na huruma
isiyo na kifani. Si mapenzi yake kwamba mtu ye yote apotee [2 Pet. 3:9; 1 Tim. 2:4; Yn.
3:16]. Katika Neno lake yeye amefanya mpango kwa kila mtu
kusafishwa na kutakaswa [Efe. 1:3-7; 1
Kor. 6:9-11]. Ahadi ya 1 Yohana 1:9 ambayo ni vigumu sana kuisadiki
inamhusu kila mwanaume, mwanamke, au mtoto katika ulimwengu huu wa leo:
“TUKIZIUNGAMA dhambi zetu, YEYE NI MWAMINIFU na wa haki hata ATUONDOLEE dhambi
zetu, na KUTUSAFISHA na udhalimu wote.”
Kwa sharti hilo la UNGAMO LA KWELI, Mungu anaahidi kuisamehe
dhambi ya aina yo yote, bila kujali ilivyo. “Haya, njoni, tusemezane, asema BWANA. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu
sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa
kama sufu.” Isaya 1:18.
Ni ahadi ya pekee ilioje hiyo kwa wale walioivunja kila
sheria ya Mungu na ya wanadamu, kwa kujitosa [kujitupa] kwao katika upotovu
kama wenda wazimu. Mungu bado angali anawapenda! Hakuna dhambi iliyo kubwa mno
kwake kuweza kushindwa kuiosha. Anangoja, mikono yake ikiwa imenyoshwa,
kumpokea mtu ye yote anayechukua hatua ya kuelekea kwenye msamaha na rehema
yake.
Picha kama hiyo ya Mungu inaonekana kuwa ni ngeni kabisa
ukiilinganisha na maneno ya Yesu katika Mathayo
12:31,32. Ikiwa Baba yuko tayari sana kusamehe na kuokoa, kwa nini,
basi, kuwe na kitu kama hicho cha dhambi isiyosameheka? Jibu lake ni rahisi.
DHAMBI HIYO HAISAMEHEKI KAMWE KWA SABABU HAIUNGAMWI KAMWE. Haitubiwi kamwe.
Mungu hatawalazimisha wenye dhambi kupokea msamaha wake. Ni lazima WATUBU
wenyewe na KUUNGAMA. Hata ile ahadi nzuri sana ya 1 Yohana 1:9 ina neno lile la
maana sana lisemalo “KAMA” [ -KI-] - “[Kama] tuKIziungama dhambi zetu….” Kwa
mamlaka ya Neno hilo la Mungu, twaweza kuhakikishiwa ya kwamba kila dhambi
itasamehewa KAMA tukiiungama kwa imani na kwa toba.
Mawazo mbalimbali yametolewa kuelezea kwa nini dhambi hiyo
moja haiungamwi kamwe. Wengine wanaamini kwamba dhambi hiyo ni ya mtu kujiua
mwenyewe; wengine wanadhani huenda ikawa ni uzinzi fulani wa kuogofya mno au
kumtukana Roho Mtakatifu.
Jambo moja ni dhahiri - hiyo ni dhambi! Huo ndio
mwanzo mzuri, kwa sababu Biblia inatoa tafsiri rahisi ya neno hilo baya sana la
“dhambi.” “Kila mtu atendaye dhambi ANAVUNJA SHERIA YA MUNGU [Amri Kumi], MAANA
DHAMBI NI UVUNJAJI WA SHERIA [Amri Kumi].” 1 Yohana 3:4, AJKK. Paulo anaupanua
usemi huo kwa kutangaza kwamba dhambi ni uvunjaji wa Sheria ile ya Amri Kumi.
“Walakini SINGALITAMBUA DHAMBI ILA KWA SHERIA [Amri Kumi]; kwa kuwa singalijua
KUTAMANI, kama torati [Sheria/Amri Kumi] isingalisema USITAMANI [Kut. 20:17].”
Warumi 7:7. Sio tu kwamba dhambi hiyo isiyosameheka inahusiana na kuivunja hiyo
Sheria Kuu ya Maadili ya Mungu [Amri Kumi], bali pia ni kosa dhidi ya Roho
Mtakatifu. Hali ya kosa hilo imefungamana kwa karibu sana na KAZI KUU ZA ROHO
huyo. Yesu alisema, “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba
atampeleka kwa jina langu, ATAWAFUNDISHA YOTE, na KUWAKUMBUSHA YOTE
niliyowaambia.” Yohana 14:26.
Mbali na kutufundisha sisi mambo yote, Yesu alidokeza kwamba
huyo Roho pia angeweza kutu“ONGOZA a[tu]tie kwenye KWELI YOTE.” Yohana 16:13.
[Kweli hiyo ni Neno na Amri Kumi – Yn. 17:17; Zab. 119:142.] Kila mwanafunzi
anayelichunguza kwa makini Neno huenda ameonja mafundisho hayo, yaani, mvuto
huo uongozao wa Roho Mtakatifu. Hapawezi kuwapo na ufahamu wa ndani wa kweli ya
Biblia bila kutiwa nuru na Roho huyo wa Mungu. Utume wa [kazi ya] tatu wa Roho
Mtakatifu ni KUTUHAKIKISHIA DHAMBI. Yesu alisema: “Yawafaa ninyi mimi niondoke,
kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda
zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo ATAUHAKIKISHA
[ATAUTHIBITISHIA] ulimwengu kwa habari ya DHAMBI [uvunjaji wa Amri Kumi], na
HAKI, na HUKUMU.” Yohana 16:7,8.
Ni kazi ya pekee ya huyo Roho kutukemea au kutuhakikishia
dhambi zetu. Mabaya yanapotendwa, DHAMIRI INACHOMWA kwa hisia ya hatia.
Tafadhali zingatia kwamba kadiri tunavyomruhusu Roho Mtakatifu KUTUFUNDISHA,
KUTUONGOZA na KUTUHAKIKISHIA DHAMBI ZETU, hatuwezi kamwe kuwa na hatia ya
kutenda dhambi hiyo isiyosameheka. Lakini hebu na tuseme kwamba sisi tunakataa
katakata kuzitambua kazi hizo tatu za Roho Mtakatifu katika maisha yetu
kuhusiana na Mungu, je, mambo yatakuwaje? Hapo ndipo mahali ambapo watu
wanaikaribia mipaka ile ya kufisha ya kutenda dhambi hiyo mbaya kuliko zote
zilizoandikwa katika kumbukumbu hizi.
Ni jambo la kuvutia sana kuchunguza kuenea kila mahali kwa
dhambi hiyo katika kumbukumbu za Biblia. Wakati fulani mmoja uliopita karibu
kila mtu katika dunia hii alikuwa amevuka mahali pale ambapo haiwezekani kurudi
nyuma. “BWANA akasema, Roho yangu [Roho wangu Mtakatifu] haitashindana na
mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka
mia na ishirini. Mwanzo 6:3. Mungu hapo anazizungumzia habari za watu wale
walioishi kabla ya ile Gharika ambao waliangamia katika gharika ile. Kwa zaidi ya
miaka mia moja Roho Mtakatifu [Roho wa
Kristo/Mungu
– Rum. 8:9; 1 Pet. 3:18-20] alikisihi sana kizazi kile kiovu kwa njia ya
mahubiri ya Nuhu [Kristo alihubiri kwa njia ya Roho wake kupitia kwa Nuhu].
Japokuwa mawazo ya moyoni mwao sikuzote yalikuwa ni mabaya tu, palikuwa na
wachache, yaani, watu wale nane waliosalia ambao waliitikia wito wa yule Roho
na kuingia katika safina ile. Wengine wote waliobaki walifagiliwa mbali na maji
yale yaliyokuwa yamechafuka vibaya sana ambayo yalikuwa yameifunika kabisa kila
inchi ya uso wa dunia hii. Baada ya miaka mingi ya kujitahidi kwa uvumilivu
mkubwa , Roho akaondoka kabisa kwao na kuwaacha wapingaji wale shupavu ili
wapate kukabiliwa na ajali waliyoichagua wenyewe.
Je, jambo hilo linaweza kutokea tena? Kuna mlandano wa
kushangaza mno kati ya siku zile za Nuhu na siku zetu hizi. Yesu alisema, “Na
kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa
Adamu [Kristo].” Luka 17:26. Kufanya mambo kupita kiasi kule kule kunatendeka
hivi sasa katika miji yote mikuu ya ulimwengu. Upotovu uliokithiri mno bado
unazionyesha waziwazi tamaa mbaya za mwili zinazofuatiwa na kila taifa chini ya
jua.
Kwa nini watu wale wengi sana walioishi kabla ya gharika
walikataa kuingia katika safina ile ya usalama? Wengi wao walimsaidia kabisa
Nuhu kuitengeneza meli ile kubwa sana. Roho Mtakatifu aliwachoma mioyo yao sana
kwa kuwahakikishia dhambi zao, lakini hawakutaka kuachana nazo na kuutii ujumbe
ule. Mwishowe Mungu akasema, “WAACHENI. Roho wangu hatashindana nao tena.”
Je, hivi kutakuwako na gharika nyingine [itakayoifunika
dunia yote]? Ni kweli kabisa. Lakini itakuwa ni GHARIKA YA MOTO, ambayo
itaiteketeza kabisa sayari hii pamoja na vyote vilivyomo ndani yake [2 Pet.
3:1-7,10]. Je, ni kwa jinsi gani ulimwengu huu unaitikia wito wa kuingia katika
safina inayowalinda na kuwaweka salama? Roho yule yule anaendelea kuwasihi sana
leo; ujumbe unaofanana na ule ambao unawatenga watu na kuwaletea uamsho unavuma
kote [2 Kor. 6:14-18; Ufu. 18:4,5; 14:6-12]; na huyo Roho wa Mungu anaendelea
kutendewa sawasawa na vile alivyotendewa katika siku zile za Nuhu.
KUMKUFURU ROHO MTAKATIFU
Nasoma mambo matatu katika Biblia ambayo watu wanayatenda
dhidi ya Roho Mtakatifu. Kwanza kabisa, katika Waefeso 4:30: “Wala
msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata
siku ya ukombozi.” Angalia kwamba watu wanaweza KUMHUZUNISHA ROHO MTAKATIFU, na
Biblia inasema kwamba itakuwa hivyo katika siku hizi za mwisho.
Ni jambo gani tena watakalofanya dhidi ya huyo mwakilishi
binafsi wa Mungu [Roho Mtakatifu]? Katika Waebrania 10:29 tunaambiwa kwamba
watu WATAMDHARAU ROHO MTAKATIFU. “Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi
mtu yule anayemkanyaga Mwana wa Mungu [kuzivunja Amri Kumi ni sawa na
kumkanyaga Kristo], na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu
ovyo, na KUFANYIA JEURI ROHO WA NEEMA?” Neno hili “jeuri” lina maana sawa na
“dharau.” Hebu basi fikiria hilo! Watamdharau Roho Mtakatifu. Basi na tuliweke
jambo moja zaidi mbele yetu. Hilo limo katika Matendo 7:51: “Enyi wenye shingo
gumu,
msiotahiriwa
mioyo wala masikio, siku zote MNAMPINGA ROHO MTAKATIFU; kama baba zenu
walivyofanya, na ninyi ni vyvyo hivyo.” Basi hapa tunayo mambo matatu ambayo
watu wanafanya ili kumkufuru Roho wa Mungu: WANAMHUZUNISHA, WANAMDHARAU, tena
WANAMPINGA kama vile walivyompinga siku zile za Nuhu [Mwa. 6:3-8].
Je, ni athari gani zinazompata mtu kwa kufanya uasi wake
wote huo dhidi ya Roho? Karibu kabisa bila ya yeye kutambua DHAMIRI YAKE
HUCHOMWA MOTO [HUUNGUZWA (Seared) – 1 Tim. 4:2, KJV], na MOYO WAKE UNAKUWA
MGUMU. Kwa kweli, hii ndiyo maana hiyo inahesabiwa kuwa ni dhambi ya kutisha.
Mara nyingine watu husema, “Sijui kwa nini Mungu aweze kuifikiria dhambi hiyo
kuwa ni kitu kibaya mno kiwezacho kufanywa.” Nitakuambia kwa nini: Kwa sababu
ROHO MTAKATIFU NDIYE NJIA YA PEKEE AMBAYO KWAYO MUNGU ANAWEZA KUMFIKIA
MWANADAMU [Yn. 16:7,8; Rum. 2:4,5; Mdo. 2:37-39; 7:54; Yak. 4:4-6].
Hakuna njia nyingine yo yote aliyo nayo Mungu ya kumwokoa
mwanadamu isipokuwa kupitia kwa Roho wake Mtakatifu. Hiyo ndiyo njia ambayo
kwayo tunaongozwa kwenye toba. Kama sisi hatunaye huyo Roho Mtakatifu, basi,
hakuna tumaini lo lote [la uzima wa milele] linalobaki kwetu [Mdo. 5:30-33;
Rum.
8:9,11,14]. Ni kama mtu anayezama baharini akiwa peke yake, halafu mtu mmoja
anakuja na kumtupia juya moja la kuokolea maisha yake. Kama mtu yule analishika
juya hilo la kuokolea maisha, basi, anaweza kuokolewa, lakini kama akikataa
kulishika juya hilo ambalo ni kiungo cha pekee na pwani kinachoweza kumpeleka
ufukoni, basi, ataangamia bila tumaini lo lote. Vile vile, sisi tumo duniani
humu, na njia ya pekee ambayo kwayo Mungu anaweza kutufikia sisi ni kupitia kwa
Roho Mtakatifu.
Kama sisi tunampa kisogo Roho wake na kukataa KUMSIKILIZA NA
KUMTII, basi, Mungu atatuacha, nasi tutapotea [Mwa. 6:3,5,7; Hosea 11:8,9;
lakini hatimaye Hosea 4:17]. Hii ndiyo maana Daudi alikuwa na wasiwasi sana
katika sala yake kuu ya toba. Alipokuwa akifichua yote yaliyo moyoni mwake kwa
Mungu katika Zaburi ya 51, Daudi alisema, “Usinitenge na uso wako, wala ROHO
[W]AKO MTAKATIFU USINIONDOLEE.” Fungu la 11. Alitambua ya kwamba endapo Mungu
angemwondoa kwake huyo Roho Mtakatifu, basi, yeye angekuwa amepotea kabisa.
Angeachwa peke yake bila kuwa na njia nyingine yo yote ya kuokolewa. Na hii
ndiyo maana Yesu alisema kwamba hiyo ndiyo dhambi isiyosameheka [kwa kuwa mtu
hawezi kabisa kutubu bila Roho – Ufu. 16:9,11,21]. Wewe unapojitenga mbali na
kukataa kumsikiliza Roho Mtakatifu, basi, hakuna tumaini lo lote kwako.
NJIA TATU ZA KUFANYA DHAMBI DHIDI YA ROHO
Hapa
nimeziorodhesha njia tatu ambazo kwazo watu wanaweza kuitenda dhambi hii [ya
kumkufuru Roho]. NJIA YA KWANZA, ni mtu kusema hivi tu, “SITAKI KUOKOLEWA;
sitaki mtu ye yote anisumbue juu ya Mungu, wala Biblia.” Si mara nyingi
utakutana na mtu kama huyo. Nafurahi kukuambia kwamba si mara nyingi. Watu
wengi sana kwa kweli wanataka kuokolewa [sio kulokoka], lakini mara kwa mara
utawakuta wengine ambao hawana hamu kabisa ya kuokolewa. Wameridhika kabisa na
mambo ya ulimwengu huu yanayokidhi tamaa zao mbaya za mwili. Hebu zingatia
isemwavyo katika Mithali 28:13. “Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; bali yeye
AZIUNGAMAYE NA KUZIACHA atapata rehema.” Wale wasiotaka kuachana na dhambi zao
hatimaye watajituliza wenyewe na kusema kwamba wanayo furaha bila kuwa na Kristo.
Hatimaye hawatasikia kushtakiwa ko kote na dhamiri zao, na Roho Mtakatifu
ATAWAACHA peke yao.
Kundi la pili ambalo linaathiriwa vibaya sana na dhambi hiyo
linaifikia kwa kupitia NJIA NYINGINE [YA PILI]. Wao wanataka kuokolewa kweli
kweli, nao wanamwambia kila mtu kwamba ni jambo walilolipa kipaumbele kwa ajili
ya maisha yao ya baadaye kuishi kwa amani na Mungu. Kwa bahati mbaya, kundi
hili linazidi KUNGOJEA UTAKAPOKUJA WAKATI MZURI UNAOFAA KUJITOA KABISA KWA
MUNGU. Wao wakiwa na nia njema yote hiyo, wanaziacha nafasi nzuri za thamani
kupita mpaka hapo nia zao zinapopooza kwa kukosa kwao uwezo wa kuamua la
kufanya. Watu kama hao bado wanaendelea kuongea juu ya kumfuata Kristo njia
yote, lakini uwezo wao wa kutenda umeharibiwa kwa KUSITA-SITA KWAO. Mwishowe
watakuwa wamechelewa-chelewa mno na kupavuka mahali pale ambapo kwao
haiwezekani kurudi nyuma.
Bila shaka kundi kubwa sana la wenye dhambi isiyosameheka
linapatikana katika kundi la tatu [NJIA YA TATU] ambalo nataka kuzungumza
habari zao. Ni ajabu ya kutosha, watu hao wanaonekana kuwa karibu hawana
mwelekeo kabisa wa kuitenda dhambi hiyo isiyosameheka. Wao ni washiriki wa
kanisa - huenda hata wamekuwa nguzo katika usharika wao. Je, hilo linakushtua
sana? Kwa nini Wakristo hao wawe katika hali ya hatari sana ya kutenda dhambi
hiyo kuliko makundi yale mengine mawili? Kwa sababu WAO HAWAJUI KWAMBA KWELI
INAZIDI KUFUNULIWA ZAIDI NA ZAIDI [Mithali 4:18]. Mamilioni ya Wakristo wamekaa
raha mustarehe katika viti vyao vyenye raha makanisani mwao wakijikinai [wakijisifu
mno] kwamba wao WAMEOKOKA. Wanajiona kwamba wao wako salama kabisa
wanapoendelea kuzifuata desturi za kanisa lao, wasitambue kwamba ubatizo ni
mwanzo tu wa safari yao ndefu ya KUKUA katika maisha yao ya Kikristo [2 Petro
3:18; Efe. 5:17; Mdo. 17:26,27,30,31].
Alisema hivi Mtunga Zaburi: “NENO lako ni TAA ya miguu
yangu, na MWANGA wa njia yangu.” Zaburi 119:105. Kadiri tunavyokwenda na
kuingia ndani zaidi katika Biblia, ndivyo kadiri zinavyozidi kufunuliwa kweli
nyingi zaidi, na ndivyo uwajibikaji wetu mbele za Mungu unavyozidi kuongezeka.
Hajamfunulia kweli yake yote mtu mmoja awaye yote kwa wakati mmoja [Yn.
16:12-15; 14:26; Mt. 28:19,20]. Taa hiyo inaangaza mbali kiasi cha kutosha
kumwezesha mtu ye yote kwenda mbele hatua moja kwa salama. Tunapopiga hatua
ile, HATUA NYINGINE INAONEKANA MBELE
YETU.
Tunapokua katika neema na maarifa, Mungu anataka sisi tuendelee kusonga mbele
kuifuata nuru ya ile kweli inayoangaza mbele yetu.
DHAMIRI INAUNGUZWA KWA KUTOTII KWETU
Basi
na tuseme kwamba mimi naiona nuru kutoka katika taa ya Neno la Mungu, lakini
NAKATAA KUITII. Hebu na tuseme kwamba Roho Mtakatifu amenichoma moyo wangu na
kunionyesha dhambi yangu [Yn. 16:8; Mdo. 2:37,38], nami najua vizuri kabisa
anachotaka kwangu, lakini mimi sipendi kabisa, tena naona haifai kuachana na
kitu hicho. Hivi kutatokea nini kwangu mimi ninapoendelea kuipuuzia nuru hiyo
na kuikataa kweli aliyonifunulia Roho - kwa msingi wa sababu yo yote ile niliyo
nayo? Naam, Roho ataendelea kusema nami, na kwa muda fulani nitaona vita ndani
ya dhamiri yangu.
Nitajisikia mnyonge na mwenye hatia. Siku zitapita, na hata
miezi itapita, wakati mimi naendelea kufanya kinyume na vile dhamiri yangu
inavyonionyesha lile lililo jema kwangu kulitenda. Taratibu, DHAMIRI YANGU
ITAANZA KUJIREKEBISHA NA KUAFIKIANA NA KILE KINACHOFANYIKA MWILINI MWANGU.
Polepole hisia zangu za dhambi zitaanza kupungua, na matendo yale ya uasi
[kutotii] kidogo kidogo yataanza kuonekana kuwa si ya kuchukiza sana.
Hatimaye, ile kweli iliyoonekana kwamba inaeleweka wazi
kabisa kwetu, wala haikuwa na utata wo wote pale mwanzo, itageuka na kuwa
dimbwi la matope la MASHAKA. Sababu mbalimbali zitajitokeza za kuhalalisha uasi
huo, na zile hisia za dhambi tulizokuwa nazo mwanzoni zitaendelea kufifia.
Maisha yatakuwa ni ya raha karibu sawa na vile yalivyokuwa kabla nuru hiyo
haijaja kwetu. Ni jambo gani litakuwa limetokea? Tutakuwa tumetenda dhambi
dhidi ya Roho Mtakatifu, nasi tutaanza kuzama na kuingia katika hali ya
kuitenda ile dhambi isiyosameheka. Unajua, DHAMBI HIYO YA KUFISHA SI TENDO LO
LOTE LILILO DHAHIRI AMBALO LINAWEZA KUTENGANISHWA NA KUTAJWA KWA JINA LAKE.
INAWEZA KUWA NI DHAMBI YO YOTE INAYOTUNZWA MOYONI baada ya kuipokea hiyo nuru
na maarifa. Hasa hasa ni HALI INAYOTOKANA NA KUFA GANZI KWA DHAMIRI
inayosababishwa na uasi wa kudumu dhidi ya ile kweli tunayoijua [Efe. 4:17-19]. Matokeo yake ni sawa
na kuipuuzia kengele ya saa. Dhamiri inageuka na kuwa katika hali ya
kustahimili kuchomwa-chomwa moyo kunakokumbusha uasi huo mpaka mwishowe,
HAITAWEZA KUTAMBUA [KUSIKIA] TENA KUCHOMWA-CHOMWA MOYO HUKO isikokutaka kabisa
ambako kunasababishwa na hatia ya dhambi ile iliyotendwa. Kama ilivyo saa,
dhamiri nayo pia inapungua nguvu yake kwa kuwa hakuna anayesikiliza tena.
Je, umeanza kuona kwamba mambo yote kwa kweli hutegemea kile
tunachofanya na ile kweli? Yakobo aliandika hivi, “Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala HAYATENDI, kwake
huyo NI DHAMBI.” Yakobo 4:17. Ni mamoja kwetu endapo sisi ni
matajiri au maskini, Wakatoliki au Wayahudi au Waprotestanti, hoja kuu inahusu
kama sisi tunatenda kile tunachokijua [Yak.
2:22; Luka 6:46-49; 11:27,28; Mt. 7:21-27].
Yesu
aliielezea kwa mapana zaidi kanuni hiyo ya maana sana. Alisema, “Kama
nisingalikuja na kusema nao, WASINGALIKUWA NA DHAMBI; lakini sasa HAWANA UDHURU
kwa dhambi yao.” Yohana 15:22. Ni nani, basi, anayewajibika na kushtakiwa mbele
za Mungu? Ni wale waliotiwa nuru na Roho Mtakatifu kutoka katika Neno lake.
Watu walio waaminifu kwa yale yote wanayoyajua, yawe mengi au machache,
watakubaliwa [na Mungu]. Dhambi itahesabiwa tu dhidi ya wale WALIOISIKIA KWELI
NA KUIKATAA KABISA [Luka 12:45-48].
Kristo alisema, “Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi;
lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa.” Yohana 9:41. Tatizo lote
hilo la dhambi hiyo isiyosameheka linazunguka katika HOJA YA UTII KWA KILE
TUNACHOKIJUA. Safari nyingine Yesu alisema, “Enendeni maadamu mnayo nuru, giza
lisije likawaweza.” Yohana 12:35. Hivi nuru hiyo inatoka wapi? Ni Roho
Mtakatifu anayetutia katika kweli yote [Yn.
16:13; 17:17; Zab. 119:142]. Sisi
tunapokataa katakata kuitii hiyo kweli, basi, tunaikataa huduma ya Roho ambaye
peke yake ndiye anayetuunganisha sisi na wokovu.
Tunamfukuza kabisa huyo Mmoja ambaye Mungu amemtuma kutuokoa
sisi. Je, waweza kuona sana jinsi jambo hili linavyoweza kumwangamiza mhusika?
Mjumbe huyo wa pekee wa Mungu anahuzunishwa na kuondoka kwa kukataa kwetu kwa
makusudi kuupokea mwaliko wake wa rehema. Hapo kale Mungu alisema, “Roho wangu
hatashindana
na mwanadamu milele [Mwa. 6:3, KJV].
Hatimaye Mungu atamwambia Roho wake Mtakatifu, atasema, “WAACHENI. Kama
wanang’ang’ania kuifuata njia yao wenyewe, usiwatafute tena.” [1 The. 5:19; Mithali 16:25.]
DINI YA WAZAZI WETU HUENDA ISIWE NZURI KIASI CHA KUTOSHA
Labda
maelezo yaliyo sahihi kabisa ya dhambi isiyosameheka katika Agano Jipya ni yale
yanayopatikana
katika Matendo 7:51: “Enyi wenye
shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, SIKU ZOTE MNAMPINGA ROHO
MTAKATIFU; kama BABA ZENU walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.” Watu
hao walipiganaje na Roho wa Mungu? Stefano anasema kwamba walifanya hivyo kwa
KUJIFICHA NYUMA YA DINI YA BABA ZAO. Wao WALIFUATA NJIA YA DINI ILE ILE TU
WALIYOPITA WAZAZI WAO. Je, kuna ubaya wo wote kwa jambo hilo? Katika mfano huo
tuliopewa palikuwa na ubaya, kwa sababu fungu hilo linaendelea kuwaeleza kama
ni wale wa“lioipokea torati (Sheria ya Mungu ya Amri Kumi) kwa agizo la
malaika, [wa]siishike.” Fungu la
Je, unaiona picha hiyo? Bila kujali wazazi wao walivyoelewa,
watu hao waliipokea Sheria [Amri Kumi] ambayo Mungu aliwataka kuitii. Kila
kizazi na kila mtu atahukumiwa kwa msingi wa KILE ANACHOKIJUA na jinsi
ANAVYOKITII. Hakuna dini ya mtu ye yote iliyo nzuri kiasi cha kutosha kwa mtu
mwingine kwa sababu kuna viwango vinavyohitilafiana vya uwajibikaji kwa kila
mtu. Babu yangu angeweza kuokolewa kwa kufuata nuru aliyokuwa nayo, lakini mimi
nisingeweza kuokolewa kwa kufanya jambo lile lile alilolifanya yeye. Mimi nina
kipimo tofauti cha ile kweli iliyokwisha kufunuliwa kwangu ambayo kwayo Mungu
atanishikilia mimi kuwa ninawajibika.
Ukweli ni kwamba mtu ye yote anamkataa na kumdharau Roho
Mtakatifu wakati ule anapoivunja kwa makusudi amri yo yote ya Mungu. Kwa mujibu
wa Biblia, Roho hawezi kukaa katika maisha ya mtu ye yote asiyetii. “Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja
na ROHO MTAKATIFU AMBAYE MUNGU AMEWAPA WOTE WAMTIIO.” Matendo 5:32. Tena, Yesu alisema: “Mkinipenda
mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine,
ili Baba, naye atawapa Msaididi Mwingine, ili akae nanyi milele.” Yohana
14:15,16.